• HABARI MPYA

  Jumanne, Novemba 29, 2016

  SIMBA, YANGA WATAKIWA KUWALIPA WADAI WAKE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imetakiwa kumlipa madai yake, kocha wake wa zamani, Mganda Amatre Richard, wakati mahasimu wao, Yanga nao wametakiwa kuwalipa wachezaji wake wa zamani, Jerry Tegete, Omega Seme na Thabit Mohammed.
  Hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyokutana Jumapili kwenye makao makuu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Kuhusu, Hamatre, Kamati imeiagiza Sekretarieti ya TFF kuandikia Simba kuhusu msimamo wa hukumu iliyotolewa kwa Simba kumlipa kocha huyo.
  Kuhusu malipo ya wachezaji Jerry Tegete, Omega Seme na Thabit Mohammed, Kamati iliamua Yanga iwalipe wachezaji hao kama uamuzi ulivyokwisha kutoka hapo awali na TFF wametakiwa kuhakikisha wachezaji hao wanalipwa. 
  Lakini madai ya mshambuliaji Said Bahanuzi dhidi ya Yanga, yamesogezwa mbele, wakati hukumu ya kesi ya Simba dhidi ya mchezaji Hassan Kessy na klabu ya Yanga inatarajiwa kutolewa wiki hii.
  Malalamiko ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Ayoub Nyenzi, Msafiri Mkemi na Hashim Abdallah yatasikilizwa mwishoni mwa wiki hii na uongozi wa klabu hiyo umeagizwa kuwasilisha nyaraka za kufukuzwa uanachama kwa Wajumbe hao.
  Uongozi wa Young Africans, chini ya Kaimu Katibu Mkuu Baraka Deusdedit umekubali kuwasilisha nyaraka hizo kabla ya kikao kijacho kinachotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii. Wenzake na Nyenzi ni Hashim Abdallah na Salum Mkemi.
  Malalamiko ya Yanga dhidi ya Kagera Sugar, wahusika kwenye shauri hili, wameamuliwa kufika Dar es Salaam mbele ya kikao kitakachoitishwa mwishoni mwa wiki ili kujieleza. Wahusika hao ni Young Africans waliowasilisha malalamiko, Panone FC ya Kilimanjaro, Kagera Sugar pamoja na mchezaji husika ili hatua stahiki zichukuliwe mara baada ya kuwasikiliza.
  Aidha, Kamati imeamua beki Said Hussein Morald sasa ni mchezaji huru baada kufikia mwafaka na klabu ya Singida United kwa barua ambazo waliwasilisha mbele ya kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA, YANGA WATAKIWA KUWALIPA WADAI WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top