• HABARI MPYA

  Jumatano, Novemba 30, 2016

  KESI YA AKINA CHACHA, MATANDIKA YAPIGWA KALENDA

  Na Hellen Mwango, DAR ES SALAAM
  KESI inayowakabili Maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesogezwa mbele hadi Desemba 5, mwaka huu baada ya jana kusikilizwa kwa mara ya pili Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam.
  Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Sosthenes Kibwengo, amesema leo mahakamani kwamba washitakiwa walirekodiwa wakati wakiomba rushwa ya Sh. milioni 25 kutoka kwa viongozi wa Chama Cha Soka Geita (GFA) ili kuisaidia timu yao kupata nafasi ya kupanda Ligi Kuu Tanzania.
  Washtakiwa hao ni Msaidizi wa Rais wa TFF, Juma Matandika na Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, Martin Chacha. Kibwengo ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo alitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi aliyepangiwa kuisikiliza.
  Martin Chacha (kulia) pamoja na Juma Matandika wanakabiliwa na mashitaka ya kuomba rushwa wakiwa TFF 

  Upande wa Jamhuri uliongozwa na Waendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Leonard Swai alyesaidiana na Odessa Horombe.
  Akiongozwa na Swai, shahidi alidai kuwa Februari 4, mwaka huu viongozi hao wa Chama cha Geita, Salum Kulunge na Constantine Morandi, walikwenda TFF kwa ajili ya kufuatilia rufani kuhusu uhalali wa usajili wa mchezaji Mohammed Jingo wa timu ya Polisi Tabora, lakini kwa sababu timu ya Geita Gold Mine ilikuwa inachuana na Polisi Tabora kuwania nafasi ya kupanda Ligi Kuu kutoka Kundi C, wakashawishiwa na Maofisa hao wa TFF kutoa rushwa ya Sh. milioni 25.
  “Mheshimiwa hakimu, washitakiwa walirekodiwa wakati wakishawishi na kuomba rushwa hiyo na walitoa mchanganuo kwamba Sh. milioni 10 watapewa Sekretarieti ya TFF, Sh. milioni 10 nyingine zitakwenda kwa Kamati ya Sheria inayohusu uhalali wa usajili wa wachezaji na Sh. milioni tano kwa ajili ya Uhamiaji wa uraia wa wachezaji... " alidai shahidi.
  Kesi hiyo itaendelea ushahidi wa Jamhuri Desemba 5, mwaka huu na upande wa Jamhuri ulidai kuwa una mashahidi 10 na vielelezo vitano dhidi ya washtakiwa.
  Katika kesi ya msingi, ilidaiwa Februali 4 mwaka huu, makao makuu ya TFF washitakiwa wakiwa waajiriwa wa shirikisho hilo, walishawishi na kuomba rushwa ya Sh. milioni 25 kutoka kwa Salum Kulunge na Constantine Morandi.
  Upande wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa Kulunge na Morandi ni maafisa kutoka Chama cha Soka Geita na klabu ya Geita Gold na kwamba washtakiwa waliomba rushwa kama kishawishi kwa TFF na Idara ya Uhamiaji Tanzania kutoa uamuzi wa dhidi ya Polisi Tabora ili kuisadia Geita kupanda Ligi Kuu. Washtakiwa walikana mashtaka hayo na wako nje kwa dhamana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KESI YA AKINA CHACHA, MATANDIKA YAPIGWA KALENDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top