• HABARI MPYA

  Jumanne, Novemba 22, 2016

  MCHEZAJI WA MKAMBA RANGERS APATA ZALI LA MKUDE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Saa 72 ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  imefuta kadi nyekundu aliyoonyeshwa mchezaji David Francis katika mchezo wa Kundi D Ligi Daraja la Kwanza kati ya timu za Mbarali United na Mkamba Rangers.
  Kamati hiyo imefuta kadi aliyoonyeshwa mchezaji huyo aliyekuwa amevalia jezi namba 5 wa Mkamba Rangers baada ya kubaini kuwa ilitolewa kimakosa. 
  Mchezaji huyo anapata bahati sawa na aliyoipata nahodha wa Simba, Jonas Mkude ambaye alionyeshwa kadi nyekundu Oktoba 1 katika mechi dhidi ya Yanga, lakini Kamati ya Saa 71 ikaifuta baada ya kubaini alionyeshwa kimakosa. 
  Jonas Mkude alionyeshwa kadi nyekundu, lakini Kamati ya Saa 72 ikaifuta

  Kundi A; Mechi namba 4 (Bulyanhulu Vs Green Warriors). Mechi hiyo haikuchezwa kutokana na wachezaji wa Bulyanhulu kutokuwa na leseni, na vilevile kutokuwepo mawasiliano kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Kamishna wa mechi hiyo juu ya tatizo hilo. Hivyo, mechi hiyo itapangiwa tarehe nyingine na kuchezwa katika uwanja huru (neutral ground).
  Mechi namba 7 (Mji Mkuu Vs Bulyanhulu). Mechi hiyo haikuchezwa baada ya wachezaji wa Bulyanhulu wakiongozwa na Katibu Mkuu wao Alphonce Innocent kugomea wakitaka wachezaji watano wa Mji Mkuu ambao hawakuwa na leseni, lakini walikuwa na utambulisho maalum kutoka TFF wasicheze.
  Licha ya Kamishna kuwataka wacheze na baadaye wawasilishe malalamiko yao kwake, walikataa huku Katibu wao Innocent akimzonga Kamishna na kumtukana. Bulyanhulu imepoteza mechi hiyo kwa kusababisha ivurugike kwa kuzingatia Kanuni ya 29(4) ambapo pia imepigwa faini ya sh. 1,000,000. Mji Mkuu imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.
  Pia Katibu Mkuu wa Bulyanhulu, Aplhonce Innocent amefungiwa miezi sita kutojihusisha na shughuli yoyote inayohusu mpira wa miguu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 29(6) ya Ligi Daraja la Kwanza.
  Kundi B; Mechi namba 1 (African Wanderers Vs AFC). Klabu ya African Wanderers imepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi licha ya kuwa ni wenyeji. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.
  Mechi namba 5 (African Wanderers Vs Kitayosce). Wachezaji Ally Rashid na Israel Said wa African Wanderers wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa Mwamuzi kuwatoa kwa kadi nyekundu baada ya kwenda nje ya uwanja na kupigana na washabiki. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Pili.
  Mechi namba 12 (JKT Oljoro Vs African Wanderers). Mechi hiyo haikuchezwa baada ya kutokea mkanganyiko wa mawasiliano kati ya African Wanderers na ofisi ya Bodi ya Ligi, hivyo itapangiwa tarehe nyingine.
  Mechi namba 2 ya Kundi D kati ya Namungo na Sabasaba. Baada ya Namungo kufunga bao, washabiki wa timu hiyo waliingia uwanjani kushangilia. Klabu hiyo pamoja na Msimamizi wa Kituo wamepewa onyo kali kuhakikisha tukio hilo halitokei tena. Pia sehemu kubwa ya uwanja huo hauna nyasi, hivyo klabu husika imetakiwa kuhakikisha nyasi zinapandwa kabla ya kuanza mzunguko wa pili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MCHEZAJI WA MKAMBA RANGERS APATA ZALI LA MKUDE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top