• HABARI MPYA

  Alhamisi, Novemba 24, 2016

  TSHABALALA AJITIA PINGU SIMBA SC HADI JUNI 2018

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ leo amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea Simba SC.
  Tshabalala mwenye umri wa miaka 21 sasa, amesaini leo ofisini kwa Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
  Na Tshabalala anaongeza mkataba Simba SC katikati ya tetesi za kutakiwa na wapinzani, Azam na Yanga. 
  Beki wa Simba SC, Mohammed Hussein 'Tshabalala' (kulia) akibadilishana fomu na Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva (kushoto) baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili leo ofisini kwa kiongozi huyo

  Tshabalala (kulia) na Aveva (kushoto) wakati wa kusaini mikataba leo Dar es Salaam

  Bado haijajulikana Simba SC imempa kiasi gani cha fedha Tshabalala kuongeza mkataba, lakini habari za ndani zinasema amesaini kwa Sh. Milioni 30.  
  Tshabalala alisaini Simba SC Juni mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar ya Misenyi mkoani Kagera, ambayo nayo ilimtoa Azam FC.
  Aliyefanikisha usajili wake kwa mara ya kwanza ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe aliyekigundua kipaji hicho.
  Hans Poppe akimzawadia gari aina ya Toyota Raum Tshabalala Septemba mwaka huu
  Tshabalala wakati anasaini mkataba wa kwanza wa kujiunga na Simba mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe (kulia) 

  Na baada ya kazi nzuri kwa misimu yake miwili ya kwanza, Poppe alimzawadia gari aina ya Toyota Raum Septemba mwaka huu.
  Mtoto huyo wa dada wa beki wa zamani wa Yanga, Said Mwaibambe Zimbwe (sasa marehemu) kwa sasa ameanza kupangwa katika kikosi cha kwanza cha Taifa Stars mbele ya beki wa Yanga, Mwinyi Hajji Mngwali.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TSHABALALA AJITIA PINGU SIMBA SC HADI JUNI 2018 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top