• HABARI MPYA

  Jumatano, Novemba 30, 2016

  BABU NGASSA AWASHAURI TOTO KUSAJILI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MENEJA wa Toto Africans, Khalfan Ngassa ameushauri wa timu hiyo kutoa fedha kusajili wachezaji wa kuiongezea nguvu timu kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Ushauri huo unafuatia kutojitokeza kwa wachezaji wa viwango vya kuridhisha katika majaribio yaliyoanza Jumatatu Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo, Ngassa kiungo wa zamani wa Pamba ya Mwanza na Simba ya Dar es Salaam, alisema kwamba aina ya wachezaji waliojitokeza hatarajii kama atapata wa kuisaidia timu katika Ligi Kuu.
  Khalfan Ngassa (kushoto) ameishauri Toto kusajili wachezaji wa kuiongezea nguvu timu kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara

  “Wamekuja wachezaji wengi sana, wanaweza kufika 60, lakini tatizo si wachezaji tayari kwa Ligi Kuu. Ni wachezaji ambao inabidi uwafanyie kazi sana. Sasa kwa wakati huu tunahitaji wachezaji wa kuisadia timu ibaki Ligi Kuu hatuna ujanja mwingine zaidi ya kutoa fedha kusajili,”alisema.
  Ngassa, baba wa mchezaji nyota nchini, Mrisho Khalfan Ngassa ambaye kwa sasa anachezea Fanja ya Oman baada ya kuwika Toto Africans, Kagera Sugar, Azam FC, Simba na Yanga za Tanzania alisema viongozi wanapaswa kusajili tu.
  “Kwa sababu hata wenyewe viongozi wameona, wale si aina ya wachezaji tunaowataka kama tunataka kubaki Ligi Kuu,”alisema.
  Toto iliburuza mkia baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kutokana na kuambulia pointi 12 katika mechi 15. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BABU NGASSA AWASHAURI TOTO KUSAJILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top