• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 26, 2016

  LWANDAMINA: NAMI NI MUUMINI WA SOKA YA PASI NYINGI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu mpya wa Yanga SC, Mzambia George Lwandamina amesema kwamba naye ni muumini wa soka la pasi nyingi, hivyo amekuja kuiongezea makali timu hiyo katika falsafa ile ile ya Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye sasa anakuwa Mkurugenzi wa Ufundi.
  Yanga imepanua benchi lake la Ufundi na sasa aliyekuwa kocha Mkuu, Pluijm anakuwa Mkurugenzi wa Ufundi, nafasi yake akimuachia Lwandamina wakati wasaidizi wanabaki kuwa Juma Mwambusi, Kocha wa makipa Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli Jacob Onyango na Mtunza Vifaa Mohamed Omar ‘Mpogolo’.
  Na akizungumza na Waandishi wa Habari jana makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam wakati wa utambulisho wa wakuu wapya wa Idara ya Ufundi, Lwandamina alisema kwamba kama ilivyokuwa kwa kocha Pluijm, naye pia ni muumini wa mchezo wa pasi nyingi.
  “Hata mimi napenda timu yangu ikae na mpira, sitaki mpira wakae nao wapinzani. Nataka tukae nao sisi, na njia pekee ya kuwazuia wapinzani wasiuchukue mpira ni kupasiana mara nyingi kadiri muwezavyo, kwa hiyo na mimi ni muumini wa mpira wa pasi nyingi,”alisema.
  Lwandamina alisema kwamba ameiona Yanga katika mechi yake ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikishinda 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting na amegundua ni timu nzuri ambayo haihitaji mchezaji mpya.
  Alisema alifurahia uchezaji wa timu haswa kiufundi wachezaji wengi wapo vizuri na sana anatarajia kuiongezea makali tu timu. “Kwetu Zambia tunacheza kwa nguvu zaidi, hapa naona ufundi zaidi, sasa ufundi ukichanganya na nguvu unakuwa vizuri sana, kwa hiyvo niseme nimekuja kuiongezea makali timu,”alisema.
  Alimsifu mtangulizi wake, Pluijm kwamba amefanya kazi nzuri na akasema atafuata nyayo zake na atashirikiana naye bega kwa bega kuhakikisha Yanga inapata mafanikio zaidi. “Lengo langu ni kuhakikisha Yanga inakuwa tishio zaidi na inafanikiwa zaidi,”alisema mwalimu huyo kutoka Zesco United ya Zambia.
  Lwandamina amekana madai kwamba amependekeza wachezaji wawili aliokuwa nao Zesco United ya kwao, Zambia kiungo Misheck Chaila na mshambuliaji Mkenya Jesse Were wasajiliwe pia. “Kama mpango huo ulikuwapo nyuma yangu, bila mimi kushirikishwa, sawa. Lakini mimi sijapendekeza mchezaji yeyote mpya,”alisema.
  Na akasema hatabadilisha kitu pia kwenye benchi la Ufundi ataendelea kufanya kazi na Maofisa wote anaowakuta na kama kutakuwa na haja ya kubadilisha mtu ni baadaye.
  Kwa upande wake, Pluijm alisema kwamba amefurahia majukumu yake mapya ndani ya Yanga na mkwa kuweka mbele maslahi ya klabu anayapokea kwa moyo mkunjufu. “Mkubwa ni klabu hapa, sisi wote tupo kwa maslahi ya klabu, sina budi kuyapokea majukumua haya mapya kwa furaha kmabisa,”.
  Makamu Mwenyekiti wa klabu, Clement Sanga kwa upande wake alisema amefurahia muungano wa Pluijm na Lwandamina jambo ambalo ni kinyume na wengi walivyotarajia.
  Sanga akasema kwamba timu itaanza mazoezi Jumatatu katika Uwanja ambao utatajwa baadaye na wote katika benchi la Ufundi watakuwapo.
  Baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 128 kwenye awamu mbili, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23, Pluijm aliyetua Jangwani mwaka 2014 anampisha Lwandamina.
  Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 110 za tangu mwaka jana, alishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.
  Na anaondoka baada ya msimu mzuri uliopita, akibeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
  Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria. Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
  Na kwa mafanikio hayo, haikuwa ajabu Pluijm akishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa msimu uliopita. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: LWANDAMINA: NAMI NI MUUMINI WA SOKA YA PASI NYINGI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top