• HABARI MPYA

  Jumatatu, Novemba 28, 2016

  BADRU: BUTUA BUTUA INAUA SOKA ZANZIBAR

  Na Salum Vuai, ZANZIBAR
  HAPANA shaka yotote kwamba mchezo wa mpira wa miguu ndio unaopendwa na mashabiki wengi zaidi kote duniani.
  Hata hivyo, kwa hapa Zanzibar, licha ya mchezo huo kuendelea kubakisha mashabiki wake wengi, kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazochelewesha kupata mafanikio.
  Kila mtu hasa miongoni mwa wadau wa soka, ana sababu zake juu ya kuporomoka kwa kiwango cha mchezo huo hapa nchini, ingawa nyengine zinafanana.
  Mohammed Badru Juma ni mwalimu wa soka mwenye uzoefu wa kufundisha timu za watoto na vijana wa chini ya miaka 20, ambaye klabu ya Tottenham Hotspurs inayocheza Ligi Kuu ya England imeuona uwezo wake na kuamua kumkabidhi akademi ya timu hiyo.
  Mohammed Badru Juma ni mwalimu wa soka mwenye uzoefu wa kufundisha timu za watoto na vijana Zanzibar

  Bin Zubeiry Sports - Online ilibahatika kuzungumza na mwalimu huyo ambaye kwa sasa yupo hapa nchini kwa shughuli zake binafsi, kuhusu anavyoiona hali ya soka la Zanzibar, changamoto zake na nini kifanyike kulipeleka mbele.
  Alianza kwa kusema ili kupata maendeleo katika mchezo wowote ni lazima kuwekeza kwa watoto wa umri mdogo, kwani wanakuwa wepesi kufundishika na kuelewa kwa haraka.   
  Badru alisema kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na vijana wengi wenye vipaji vya hali ya juu katika mchezo wa mpira wa miguu, lakini hata hivyo, alisema vinahitaji kukuzwa kwa kutumia mifumo madhubuti na ya kisasa.
  Alieleza kuwa alichokigundua katika timu za vijana hapa Zanzibar, ni wachezaji wa timu mbalimbali kucheza kwa kuonesha vipaji binafsi, lakini hawaoneshi kama kuna vitu vipya wanavyofundishwa.
  “Napata wasiwasi labda walimu wengi wenye leseni za ngazi mbalimbali hawatumii taaluma wanayopata katika kozi na vyeti vyao vinabakia makabatini na havitumiki kuzalisha matunda yanayotarajiwa,” alieleza.
  Alisema suala la ufundi ni tatizo la walimu wengi, ambapo katika kuwaangalia kwake kwenye mazoezi au mechi mbalimbali, amebaini kuwa hawafundishi mifumo na jinsi ya kuucheza mpira.
  Katika hali kama hii, Badru alisema timu zinafanya vibaya ingawa zina walimu waliosomea na kutunukiwa vyeti, kwa kuwa walimu hawajishughulishi kuwafundisha na kuwakuza vijana badala ya kutegemea tu uwezo wao binafsi waliojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
  Alifahamisha kuwa, vijana wanapoitwa kwenye timu wanakuwa tayari wana vipaji na uwezo binafsi, na kinachohitajika sasa ni walimu kuukuza uwezo huo kwa kuwapa mbinu za kucheza mpira.
  Kocha huyo alisema katika mechi nyingi anazohudhuria hasa uwanja wa Amaan, hajaona wachezaji kuonesha ufundi wa kucheza na mpira jambo alilosema linawafanya wabutuebutue kwa presha ya kutafuta magoli.
  Alisema ingawa soka linahitaji matokeo ambayo huja kwa kufunga magoli, lakini lazima wachezaji wafunzwe namna ya kumiliki mpira, kuusarifu na kuonesha vitu vya kufurahisha mashabiki.
  Badru alisema, mbali na umuhimu wa kufunga magoli ili kupata ushindi, lakini soka pia ni mchezo wa burudani.
  Kwa hivyo alisema ni muhimu magoli hayo yapatikane kutokana na ufundi unaoleta raha mchezoni badala ya kupiga mipira mbele ili kuzifumania nyavu.
  Katika hili, alisema ni jukumu la mwalimu kuwafundisha mifumo ya uchezaji anayoitaka  badala ya kuwaachia wachezaji kucheza wajuavyo wao huku wakiharakia kufunga.
  “Ni kweli mashabiki wanataka timu zao zishinde lakini ni wajibu wa mwalimu na wachezaji kuwapa burudani kwa kuhakikisha wanatumia muda mwingi kuonesha ufundi wa kujipanga, kucheza, na kukaa na mpira kwa muda mrefu huku wakionesha vitu adimu na vinavyoweza kukonga nyoyo,” alifahamisha Badru.
  Hili, alisema linahitaji uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility) kati ya wachezaji wote uwanjani, na si busara mwalimu kumuangalia mchezaji mmoja mmoja kwa kutegemea uhodari wao ili wakafunge magoli.
  Alitoa mfano wa mechi ya kirafiki kati ya timu za mtaa mmoja wa Jang’ombe zenye upinzani mkubwa wa kisoka, Taifa na Jang’ombe Boys uliochezwa wiki iliyopita.
  Anauzungumziaje mchezo huo uliovunja rekodi ya kujaza uwanja pomoni?   
  Alisema pamoja na uwanja kujaa kupindukia, lakini mchezo wa uwanjani ulikuwa wa kawaida, na wachezaji hawakuwa wakionesha burudani ya kuusarifu mpira wala kumiliki.
  Alisema katika mchezo kama ule, wachezaji walipaswa kuwatendea haki maelfu ya mashabiki waliohudhuria, kwa kuonesha hasa kiwango cha kucheza badala ya kuusukuma mpira kwa lengo la kufunga magoli.   
  “Ninawapongeza Taifa kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys, lakini kwa mchezo niliouona, nasikitika kusema kwamba soka la Zanzibar lina safari ndefu kama tunataka tubadilishe nafsi za mashabiki ili warudi kuzipenda timu za kwao,” alisema.  
  Kuhusu changamoto ya viwanja vinavyotumika kwa mechi za ligi za madaraja mbalimbali Zanzibar kutokuwa na viwango vinavyowapa wachezaji nafasi ya kujidai, Badru alisema hilo si tatizo kwani kocha anatakiwa aandae aina ya mchezo kulingana na hali ya uwanja utakaotumika.
  Kwa mfano, alisema mechi inapochezwa katika viwanja vilivyoko nje ya mji kama ule wa Fuoni, hapo lazima kocha asome mazingira ya uwanja huo na hatalazimika kutaka kumiliki na kucheza mpira wa burudani, bali ataharakisha kufunga ili ushindi upatikane.   
  “Lakini ninashangaa pale timu zinapocheza katika viwanja vya Amaan au Gombani ambavyo vinaruhusu kubaki na mpira muda mrefu, kuucheza kwa matakwa ya timu, lakini bado tunashuhudia butuabutua,” alieleza Badru.
  “Kwani unadhani watu wanapenda soka la Ulaya kwa sababu gani? Ni burudani bila shaka, si unaona klabu kama Barcelona yenye mafundi wa kila aina wanaoweza kucheza na mpira jinsi wanavyowapa raha mashabiki?.
  “Timu inashinda lakini magoli yanakuwa matamu kwa uwezo wa ku- ‘possess’ (kumiliki) mpira na kuwazungusha wapinzani, sio kupiga mbele tu ili mradi liende” alifafanua Badru.     
  Badru pia alitoa mfano wa klabu za Small Simba, Malindi SC, Black Fighters, Mlandege na nyengine zilizotamba zamani, akisema zilifanikiwa kuvuta mashabiki hata kutoka mashamba kuja mjini siku zilipokuwa zikicheza.  
  Alisema hilo lilitokana na hayo aliyotangulia kueleza, ambapo walimu wa miaka hiyo walijua mbinu na wachezaji walifahamu wajibu wao wawapo uwanjani.
  Alieleza kuwa, wakati huo, sio watu wote waliokuwa na timu za kushabikia, lakini walikuwa wakienda viwanjani kwa kuvutiwa na raha ya soka la ukweli.
  Katika hali kama hiyo, Badru alisema hata kama shabiki timu yake ilifungwa, ingawa aliumia lakini hufurahia na kupiga makofi kwa jinsi magoli yalivyokuwa yakitengenezwa kitaalamu.   
  “Sasa hayo hayapo na watu wamevifanya viwanja vya soka kama baraza ya kwenda kupotezea wakati na kula njugu na juice kwa kuwa hawana pa kwenda,” alisema Badru ambaye kaka yake Hafidh Badru, ndie kocha pekee hadi sasa aliyeleta kombe la Chalenji Zanzibar mwaka 1995.
  Nini kifanyike ili kuondokana na mkwamo huo? 
  Akijibu suala hili, alisema walimu wafanye hadidu rejea za mafunzo wanayopata kila mara na kujifunza zaidi  namna ya kuzijenga timu za watoto wadogo ambao ndio msingi wa timu bora za hapo baadae.
  Lakini alisema, hilo litawezekana iwapo Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kitakuwa na mfumo mzuri wa kuwashirikisha wadau wa soka wakiwemo wachezaji wa zamani, ili kujua siri ya mafanikio yao na vipi wataweza japo kwa ushauri kusaidia soka la Zanzibar lisiende arijojo.
   “Kama msemo wa Kiswahili usemavyo ‘Mkongwe hagewa’, ZFA pia inapaswa kulijua hili na kuwasogeza karibu nao wachezaji wa zamani ambao katika nchi nyengine, husaidia sana kuinua mchezo wa mpira wa miguu,” alihitimisha.
  Kwa kipindi alichokuwepo nchini akiwa mapumzikoni, Mohammed Badru aliombwa kuisaidia JKU ambayo kocha wake mkuu Malale Hamsini alitimkia JKT Ruvu Tanzania Bara na kukaa benchi katika mechi tano za mwisho kabla hajapanda ndege kurejea Uingereza.
  Baadae alikuja tena Zanzibar na msimu huu pia ameombwa kuichukua timu hiyo na ameiacha ikiwa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi kuu, huku akikabidhiwa jukumu jengine la kuinoa timu ya Raskazone inayocheza ligi daraja la pili Wilaya ya Mjini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BADRU: BUTUA BUTUA INAUA SOKA ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top