• HABARI MPYA

    Monday, November 28, 2016

    MBELE KWA MBELE SAMATTA, HAINA KUFELI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    ILIKUWA vigumu kidogo kuamini mchezaji mpya kabisa barani Ulaya anaingia kwenye timu na moja kwa moja kuanza kucheza kwenye kikosi cha kwanza, tena mashindano yote ya ndani hadi Ulaya.
    Hiyo ndiyo ngekewa aliyoingia mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji Janauri mwaka huu.
    Samatta alianza taratibu kwa kupewa dakika chache kutokea kwenye benchi, lakini baada ya kufunga mfululizo, kocha Mbelgiji, Peter Maes akamuamini kijana huyo mzaliwa Mbagala, Dar es Salaam.
    Mbwana Samatta (kushoto) jana amecheza mechi ya 35 tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC
    Samatta akiwa na mshambuliaji wa Borussia Dortmund ya Ujerumani, Pierre-Emerick Emiliano François Aubameyang ambaye pia ndiye Mwanasoka Bora wa Afrika Januari mwaka huu nchini Nigeria walipokwenda kupokea tuzo zao
    Hata hivyo, baada ya mwanzo mzuri Ulaya, Samatta akaingia katika wakati mgumu kidogo kufuatia kupoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
    Kwa mara ya pili mfululizo, Alhamisi iliyopita Samatta alitokea benchi kumalizia dakika tano za mwisho KRC Genk ikishinda 1-0 dhidi ya Rapid Viena katika mchezo wa Kundi F Europa League Uwanja wa Laminus Arena, Genk.
    Kwa matokeo hayo, Genk imefuzu hatua ya mtoano baada ya kupaa kileleni mwa Kundi F kwa pointi zake tisa, sawa na Athletic Bilbao ya Hispania. Genk imeongoza kwa wastani wa mabao, wakati Rapid Viena imemaliza nafasi ya tatu na pointi tano sawa na Sassuolo ya Italia iliyoshika mkia.
    Samatta aliingia uwanjani dakika ya 85 kuchukua nafasi ya mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis katika mchezo ambao bao pekee la Genk lilifungwa na mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis dakika ya 11.
    Katika mahojiano na Bin Zubeiry Sports – Online baada ya mchezo huo, Nahodha huyo wa Tanzania,  alisema kwamba yupo katika wakati mgumu kwa sasa na anahitaji kupambana kurudisha nafasi yake katika kikosi cha kwanza Genk.
    Samatta amekuwa mkweli na muwazi akisema kwamba mshindani wake wa namba, Nikolaos Karelis kwa sasa anafanya vizuri zaidi yake.” Tunayecheza naye nafasi moja anafanya vizuri, Nico Karelis yuko kwenye fomu nzuri anafunga karibu kila mechi, kwa hivyo anastahili kuanza mechi,”alisema akizungumza kwa simu kutoka Ubelgiji.        
    Hata hivyo, jana Samatta amecheza dakika zote 90, lakini timu yake KRC Genk imefungwa mabao 6-0 na KV Oostende katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji.
    Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Versluys Arena mjini Oostende, Genk ilicheza pungufu baada ya mshambuliaji wake Mjamaica, Leon Bailey kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 68.
    Mabao ya Oostende yalifungwa na kiungo Muargentina Franck Berrier dakika ya 19, beki Mcroatia, Antonio Milic dakika ya 29, mshambuliaji Mzimbabwe, Knowledge Musona dakika ya 56, mshambuliaji Landry Nany Dimata kutoka DRC mawili dakika ya 71 na 86 na mshambuliaji Muivory Coast, Gohi Bi Zoro Cyriac dakika ya 83.
    Huu ulikuwa mchezo wa kwanza Samatta kuanza baada ya mechi tatu mfululizo za kutokea benchi tangu alipoanza mara ya mwisho Novemba 3 dhidi ya Athletic Bilbao kwenye Europa League.
    Mshambuliaji Mgiriki, Nicolous Karelis aliyekuwa anaanza mechi zilizopita mbele ya Samatta jana alikuwa benchi muda wote.
    Makali ya Samatta yalianza kupungua baada ya kuumia kwenye mchezo wa Europa League dhidi ya Rapid Wien ya Austria Septemba 15, mwaka huu Genk ikishinda 3-2 Uwnja wa Laminus Arena.
    Na siku hiyo, Samatta alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia na kutoka dakika ya 78, nafasi yake ikichukuliwa na Karelis. 
    Samatta alikaa nje kwa wiki tatu na tangu hapo hata baada ya kurejea hakupata nafasi ya kuanza kutokana Karelis kufanya vizuri kabla ya kurejea jana.
    Jana Samatta amecheza mechi ya 35 tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, 18 msimu uliopita na 15 msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.
    Katika mechi hizo, ni 18 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na sita msimu huu, wakati 16 alitokea benchi nane msimu uliopita na 13 msimu huu – na mechi 10 hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na nne msimu huu.
    Ikumbukwe Samatta alitua Genk Januari mwaka huu kwa mkataba wa miaka minne akitokea kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na Mazembe na pia kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika baada ya kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa.
    Wazi bado ana safari ndefu na wakati anaokutana nao sasa ni changamoto nzuri ya kupandisha kiwango chake. Wanasoka wengi nyota wa zamani na wa sasa katika historia zao kuna kipndi kama anachopitia Samatta.
    Nini anaopaswa kufanya nyota huyo wa Tanzania? Bidii ya mazoezi, kufanyia kazi makosa na mapungufu yake – hapana shaka atarudisha nafasi yake na atang’ara zaidi Ulaya na kutimiza ndoto zake. 
    Kama anavyosema mwenyewe, haina kufeli, basi apambane kweli ili asifeli. Mbele kwa mbele Poppa!  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBELE KWA MBELE SAMATTA, HAINA KUFELI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top