• HABARI MPYA

    Sunday, February 07, 2016

    HANS POPPE ATAIJENGEA KWELI SIMBA UWANJA, AU POROJO KAMA ZA MANJI?

    TOVUTI namba moja ya michezo nchini, BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana imetoa picha zikiwaonyesha Rais wa Simba SC, Evans Aveva na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe wakiwa na Mhandisi kwenye kiwanja cha klabu, Bunju, Dar es Salaam.
    Na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE ambayo inaongoza kusomwa na watu wengi nchini, ikamnukuu Hans Poppe akisema kwamba Mhandisi huyo amekwenda hapo kwa ajili ya kutathmini uwekaji nyasi bandia.
    Alisema nyasi bandia zimekwishaagizwa na zinatarajiwa kuwasili nchini kuanzia Machi kutoka China, ili ziwekwe na Uwanja huo uanze kutumika kwa mazoezi ya timu.

    Ni hatua nzuri ya kupongeza – kwamba kwa mara ya kwanza katika historia yake tangu kuanzishwa kwake takriban miaka 80 iliyopita, Simba SC sasa inaelekea kuwa na Uwanja wake.
    Wapinzani wao wa jadi, Yanga SC wamekuwa na Uwanja wao, Kaunda kwa muda mrefu, ingawa miaka ya karibuni wameutelekeza na wamerudia kuazima viwanja vya mazoezi.
    Picha za Poppe na Aveva wakiwa na Mhandisi Frank zimetazamwa na maelfu ya wapenzi wa Simba SC na bila shaka wamepokea vizuri mpango huo.
    Mapema mwezi huu, Hans Poppe aliahidi kuijenga Uwanja wa mazoezi klabu hiyo kwa mapenzi yake, akisema kwamba amekuwa akiumia sana kuona Simba SC inahangaikia Uwanja wa kufanyia mazoezi wakati tayari ina eneo lake Bunju.
    “Nilikaa nikatafakari gharama za ujezi wa Uwanja mzuri wa mazoezi, nikaona ninaweza kuifanyia kitu hiki klabu yangu. Na sasa nipo katika mchakato wa kuanza ujenzi muda si mrefu,”alisema Poppe.
    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba anataka Simba SC iondokane kabisa na tatizo la Uwanja wa mazoezi.
     “Sitapenda kuendelea kuona tunahangaikia Uwanja wa mazoezi, ndiyo maana nimeamua kujitolea kwa mapenzi yangu kuwajengea Uwanja wa mazoezi,”alisema.
    Na baada ya kauli hiyo, kuonekana katika picha akiwa na Mhandisi kwenye eneo la kiwanja cha klabu maana yake ni hatua moja mbele kuelekea kwenye mradi huo.
    Kadhalika na kwa kinywa chake Hans Poppe kusema nyasi zimekwishaagizwa kutoka China na zinatarajiwa  kuwasili nchini kuanzia Machi, maana yake zoezi la ujenzi wa Uwanja wa Simba liko mbioni kuanza.
    Hapa Dar es Salaam, timu yenye Uwanja wake wenye viwango vilivyothibitishwa kwa mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na la Kimataifa (FIFA) ni Azam FC pekee, timu iliyoanzishwa takriban miaka 10 iliyopita.
    Yanga SC wamekuwa na Uwanja mapema sana, tena katikati ya Jiji – lakini hawakuweza kuuendeleza na mbaya zaidi wameuacha umeharibika.
    Mwenyekiti wa sasa wa Yanga SC, Yussuf Manji aliahidi kuukarabati Uwanja wa Kaunda na uwe wa kisasa, lakini ameshindwa kutekeleza ahadi hiyo.
    Manji ameshindwa kuisaidia Yanga SC angalau iwe na Uwanja wa mazoezi tu, badala yake imekuwa ikitumia fedha nyingi kukodisha viwanja vya kufanyia mazoezi.
    Simba SC sasa wamepata matumaini mapya baada ya kuwaona Hans Poppe na Aveva wakiwa na Mhandisi katika eneo la kiwanja cha klabu, Bunju.
    Na bila shaka kwa ahadi ya nyasi kuwasili kuanzia Machi, wapenzi na wanachama wa Simba SC wamefurahi mno na sasa wanaanza kuhesabu siku.
    Wanahesabu siku kuelekea Machi ili waone nyasi bandia zitakavyowasili – na baada ya hapo, kusikilizia ujenzi wa Uwanja.
    Kuna msemo mmoja usemamo; “Hata mbuyu ulianza kama mchicha” – nataka kuwaambia wana Simba SC kwamba kama viongozi wao wana nia ya dhati, basi ipo siku klabu itakuwa na Uwanja wa maana.
    Hans Poppe na Aveva wanapaswa kufahamu kwamba wana Simba SC wana kiu ya maendeleo ya ndani na nje ya Uwanja kwa klabu yao.
    Wanatamani kuisikia Simba SC inatajwa katika kila zuri, inakuwa mfano kwa mafanikio ya uwanjani na nje ya Uwanja.
    Na wana Simba SC wamechoka na ahadi zisizotimizwa kwa miaka sasa, kiasi kwamba wamekwishaanza kukata tamaa.
    Kukata tamaa ni hatua mbaya ambayo kwa watu waliokwenda shule kama Hans Poppe na Aveva wanajua maana yake – na bila shaka wanafahamu si vyema kuwafikisha wana Simba kwenye kukata tamaa.
    Hans Poppe na Aveva wanatakiwa kujua kwamba muda wa maigizo umekwishapita na sasa ni wakati wa kufanya kweli, iwe kweli watu waone kweli yametimia.
    Na wajue kwamba, kuanzia sasa watu wataanza kuhesabu siku kuelekea Machi kulingana na ahadi za ujio wa nyasi – ili wajue kwamba ahadi ya Hans Poppe ni kweli, au porojo kama za Manji?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE ATAIJENGEA KWELI SIMBA UWANJA, AU POROJO KAMA ZA MANJI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top