• HABARI MPYA

    Friday, May 08, 2015

    HII NDIYO AFRIKA, DOLA 800,000 POSHO ZA WACHEZAJI IVORY COAST WALIOSHINDA AFCON ZALIWA

    Abidjan, IVORY COAST
    MAMLAKA nchini Ivory Coast imethibitisha dola za Kimarekani 800,000 zimepotea kutoka katika posho za wachezaji waliotwaa Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Equatorial Guinea Februari mwaka huu.
    Meneja Uhasibu wa Taifa alifukuzwa kazi Jumatano baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani kufungua uchunguzi wa kashfa hiyo.
    Wizara ya Michezo na Shirikisho la Soka wamekuwa wakinyoosheana vidole tangu mwezi uliopita baada ya wachezaji kufichua kwamba hawakulipwa posho zao ipasavyo.

    Baada ya kurejea kutoka kwenye AFCON ya 2015, kila mchezaji aliahidiwa dola za Kimarekani 97,000 (dola 50,000 nyumba pamoja na fedha taslimu dola 47,000).
    Kocha Herve Renard angekunja dola 123,000 wakati fedha nyingine dola 490,000 wangegawana watu wengine wa benchi la Ufundi.
    Pamoja na hayo, kiungo wa VfB Stuttgart, Serey Die alisema mapema Aprili kwamba walipewa fedha kidogo tu na kocha Mfaransa, Renard akathibitisha kwamba hakupata haki yake.
    Serikali imeamua kulivalia njuga suala hilo wiki hii, kufuatia Wazara ya Michezo na Shirikisho la Soka kushindwa kulitatua.
    Wakiongozwa na nyota kama Nahodha, Yaya Toure, Gervinho na wengine Tembo wa Ivory Coast waliifunga Ghana katika fainali na kutwaa taji hilo kwa mara ya pili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HII NDIYO AFRIKA, DOLA 800,000 POSHO ZA WACHEZAJI IVORY COAST WALIOSHINDA AFCON ZALIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top