• HABARI MPYA

    Wednesday, February 11, 2015

    YALIYOMKUTA MRISHO NGASSA NI FUNDISHIO KWA WACHEZAJI WENGINE

    MWISHONI mwa wiki, mshambuliaji nyota Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa alitoa dukuduku lake, baada ya kuelezea namna ambavyo klabu yake, Yanga SC inamuathiri kisaikolojia.
    Baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ngassa akatoa ya moyoni Jumapili.
    Akasema, anajuta kukataa ofa nzuri ya kwenda kucheza El Merreikh ya Sudan mwaka juzi kwa kuendekeza matakwa ya nafsi yake, iliyomshawishi arejee Yanga SC.
    Akasema kufikia kujuta ni baada ya klabu yake, Yanga SC kukiuka makubaliano naye kuhusu deni la mkopo wa benki iliyomshawishi kuchukua alipe deni la Simba.

    Iko hivi, Ngassa alitolewa kwa mkopo Simba SC kutoka Azam FC akiwa katika msimu wake wa mwisho kimkataba- na wakati huo mwaka 2012, Ngassa mwenyewe alitaka sana arudishwe Yanga.
    Lakini kwa sababu uongozi wa Azam FC ulikerwa na kitendo cha mchezaji huyo kwenda kubusu jezi ya Yanga baada ya kuifungia bao pekee la ushindi timu hiyo katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DRC.
    Kwa furaha yake, Ngassa akaenda kwa mashabiki wa Yanga SC na kumpokonya shabiki mmoja jezi akaibusu. Uongozi wa Azam ukamuambia kocha wa wakati huo, Stewart Hall asimpange Ngassa katika mchezo wa fainali na Yanga baada ya kitendo alichofanya katika Nusu Fainali.
    Stewart Hall akawakatalia, akasema hawezi kuacha kumpanga mchezaji aliyefunga bao lililoipeleka timu fainali- na kweli akampanga Azam FC ikafungwa 2-0 na Yanga SC.
    Kilichofuata, Stewart akatupiwa virago na Azam FC ikatangaza kumuuza Ngassa, ikisema klabu yoyote yenye ofa ya Sh Milioni 50,000 ijitokeze kumchukua.
    Baadaye Azam FC ikatangaza kumuuza kwa mkopo Ngassa Simba SC, kufuatia kukubaliana kwa bei ya Sh Milioni 25,000.
    Lakini Ngassa mwenyewe akaibuka, akisema hayuko tayari kuuzwa kama mzigo, anataka ahusishwe katika makubaliano naye aridhie.
    Simba SC wakamtafuta Ngassa wakazungumza naye na kufikia makubaliano, akasaini. Alipewa gari aina ya Verosa na Sh. Milioni 18, zote jumla thamani yake Milioni 35.
    Wakati huo, ilielezwa kwamba alipewa gari na fedha hizo ili akubali kwenda kucheza kwa mkopo, lakini mwishoni mwa Mkataba baada ya kuanza tetesi kwamba mchezaji huyo amekwishasaini Mkataba wa kurejea Yanga SC, Simba SC wakasema Ngassa alisaini nao Mkataba mpya wa mwaka mmoja zaidi.
    Wakati Mkataba wake wa mkopo unaelekea ukingoni Simba SC, El Merreikh ikaja na ofa nzuri, kumnunua kwa dola za Kimarekani 100,000- kumpa yeye mwenyewe mchezaji dola 100,000, mshahara wa dola 6,000 kwa mwezi katika Mkataba wa miaka mitatu.
    Ajabu iliyowastaajabisha wengi, Ngassa alikataa. Wengi tulijiuliza katika maisha yake Ngassa anataka nini?
    Baada ya hapo, Ngassa akaibukia Yanga SC, akasaini timu yake ya zamani kwa mbwembwe- Simba SC ikafufua madai ya fedha zake, Sh Milioni 35.
    Japokuwa mchezaji alikuwa anakataa kuongeza Mkataba, kesi ilipofika Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakati huo chini ya Mwenyekiti Wakili Alex Mgongolwa, mchezaji akakutwa na hatia ya kuongeza Mkataba kweli na kutakiwa kurejesha Milioni 35 na fidia ya Sh Milioni 10, jumla Sh, Milioni 45.
    Yanga SC wakamshawishi Ngassa achukue mkopo benki kulipa fedha hizo, halafu yeye atakuwa anakatwa taratibu katika mshahara wake.
    Kwa mujibu wa Ngassa, makubaliano ya awali, ilikuwa awe anakatwa Sh. 500,000 kwa mwezi, baadaye ikapanda hadi Milioni 1 kwa mwezi, naye hakujali.
    Lakini imefika sasa mshahara wake wote unapelekwa benki. Na mbaya zaidi, anasema kuna baadhi ya fedha alikuwa anakatwa, lakini hazifiki benki.
    Fikiria, baada ya mwaka na nusu wa kukatwa, deni la Sh, Milioni 45 zimepungua Sh. Milioni mbili tu, Ngassa bado anadaiwa Sh. Milioni 43 na CDRB.
    Mwezi huu ambao mabao yake yanaiweka kileleni mwa Ligi Kuu Yanga SC, Ngassa anapiga miayo- kwani hakupata mshahara mwezi uliopita.
    Hadi kuja kufikia kuzungumza hadharani, Ngassa amekaa nayo sana moyoni na ametafuta njia nyingi za kumaliza tatizo hilo bila mwafaka.
    Yanga SC si mbaya. Tatizo kuna watu wamepewa dhamana pale Yanga SC ndiyo wabaya, tena huwezi kuwadhania. Hawajui kuishi na wachezaji na kwa watu wa aina ile, ni vigumu timu kuwa katika kiwango ambacho mashabiki wanataka.
    Kesi ya Mganda Emmanuel Okwi ilikuja, ikapita na TFF ilibaini Yanga SC walikuwa wana makosa. Mashabiki wakajenga chuki za bure na Okwi, lakini ukweli ni kwamba ukizama ndani kwenye sakata hilo, Mganda huyo alikuwa ana dhamira ya kweli ya kuchezea timu hiyo, bali matatizo ya viongozi ya wa klabu, yalimfanya aende kusaini bure timu yake ya zamani, Simba SC.
    Wachezaji wengi pale Yanga SC wana matatizo yanayowasababishia msongo wa mawazo na ndiyo maana viwango vinashuka.
    Jiulize, mtu kama Mrisho Ngassa kwa mazingira haya, anawezaje kucheza vizuri- ikiwa miezi mitatu mshahara hana, anakatwa fedha mwaka na nusu kila mwezi Milioni 1, kakini anakuja kugundua kalipa Milioni 2 tu. 
    Said Bahanuzi ‘anakufa na yake moyoni’- alipoteza makali kabisa Yanga SC, lakini katolewa kwa mkopo tu Polisi Moro ameanza kufunga tena.
    Sote tunafahamu fedha za mpira hatulipani kwa mikopo ya benki yenye riba kubwa, tunalipana kwa kukatana katana kwenye mapato yanayotokana na mchezo wenyewe.
    Kwa nini sasa Ngassa alipelekwa kuchukua mkopo benki? Upande mwingine, kwa Ngassa ni matatizo ya kujitakia, kuacha ofa nzuri Merreikh kukimbilia shida na matatizo Jangwani na hilo ni fundisho kwa wachezaji wengine pia. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YALIYOMKUTA MRISHO NGASSA NI FUNDISHIO KWA WACHEZAJI WENGINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top