• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 26, 2015

  CHIDDY BENZ AHUKUMIWA MIAKA MIWILI JELA

  MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam, imemhukumu Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Rashid Makwaro (29), maarufa kama Chid Benz kulipa faini ya Sh. 900,000 au kwenda jela miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na Dawa za kulevya.
  Chid Benz alikuwa anakabiliwa na mashitaka matatu ikiwamo kukutwa na  Heroin zenye thamani ya Sh. 38,638, bangi ya Sh. 1,720 na vifaa ya kuvutia dawa hizo kijiko na kigae.
  Akisoma hukumu hiyo leo, Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema, alisema baada ya mshtakiwa kukiri mashitaka yake mahakama imemtia hatiani na kuona anastahili adhabu hiyo.  Chiddy Benz amenusurika kwenda jela baada ya kulipa faini ya Sh. 900,000

  Kabla ya kusoma hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Diana Lukondo, alidai kuwa baada ya mshtakiwa kukiri mashitaka yake upande wa Jamhuri unaomba kuwasilisha dawa hizo na vifaa alivyokutwa navyo  mahakamani kama kielelezo.
  Mshtakiwa hakuwa na pingamizi ya dawa hizo kupokelewa mahakamani. Pia, Lukondo alidai kuwa mshitakiwa katika maelezo yake ya awali alipohojiwa na Polisi alikiri kukutwa na dawa hizo pamoja na vifaa vya kuvutia.
  Mahakama ilipokea vielelezo hivyo katika kesi hiyo na ilimtaka kujitetea ili apunguziwe adhabu.
  “Mheshimiwa hakimu naomba mahakama inisamehe kwa sababu nitatumia nafasi hii kuacha dawa za kulevya na kuwafundisha vijana wenzangu kupitia usanii wangu kwamba kutumia dawa hizo ni kosa la jinai,” alidai Chid Benz wakati akiomba kupunguziwa adhabu yake.
  Hakimu Lema alisema kwa kuwa mshtakiwa amekiri kwa hiyari yake, mahakama inamtia hatiani kwa makosa yote matatu.
  Alisema mahakama inamhukumu mshtakiwa kulipa faini ya Sh. 300,000 kwa kila kosa akishindwa atakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka miwili. Hata hivyo, Chid Benz alilipa faini hiyo na kuachiwa huru.
  Katika kesi ya msingi, msanii huyo alidaiwa kuwa Oktoba 24, mwaka jana katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, uliopo Ilala mjini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa na dawa za kulevya aina ya heroin kinyume na sheria zenye uzito wa gramu 0.85.
  Ilidaiwa kuwa katika shitaka la pili, siku na eneo la tukio la kwanza, mshtakiwa alikutwa na gramu 1.72 za bangi kinyume na sheria.
  Wakili huyo wa serikali alidai kuwa, siku na eneo la tukio la kwanza na la pili, mshtakiwa alikutwa pia na akiwa na vifaa vinavyotumika kuvua dawa za kulevya aina ya heroin, kigae na kijiko huku akijua ni kosa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHIDDY BENZ AHUKUMIWA MIAKA MIWILI JELA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top