• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 21, 2015

  ABDI KASSIM ‘BABBI’ ALIPA KISASI KWA DIOUF, AMTANDIKA 2-1 MALAYSIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MACHI 24, mwaka 2007, akiwa Nahodha wa Senegal, mshambuliaji El Hadji Ousseynou Diouf aliwaongoza Simba wa Teranga kuwafunga Tanzania mabao 4-0 Uwanja wa Leopold Sedar Senghor mjini Dakar.
  Taifa Stars iliyoongozwa na kiungo mshambuliaji mwenye mashuti makali, Abdi Kassim Sadallah ‘Babbi’ ilipata kipigo hicho katika mchezo wa Kundi la saba kuwania tiketi za kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2008 nchini Ghana.
  Siku hiyo, Mamadou Niang katika ubora wake, peke yake alifunga mabao matatu katika dakika za 35, 49 na 64, huku bao lingine likifungwa na Diomansy Kamara dakika ya 46.
  Kiungo wa Tanzania, Abdi Kassim 'Babbi' akimiliki mpira mbele ya Msenegali, El Hadji Diouf (nyuma kulia) na wachezaji wengine wa Sabah katika mchezo wa Ligi Kuu ya Malaysia jana

  Katika mchezo wa marudiano, Babbi alishindwa kuiongoza Taifa Stars kulipa kisasi mbele ya Simba wa Teranga, Juni 2, mwaka 2007 baada ya sare ya 1-1 Uwanja wa Kirumba, Mwanza, siku ambayo Diouf na Niang walibaki Ulaya.
  Tanzania, wakati huo chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo ilianza kupata bao kupitia kwa Nizar Khalfan dakika ya 18, kabla ya Demba Ba akiwa ‘hajulikani bado’ kuisawazishia Senegal dakika ya 75.
  Miaka nane baadaye, Diofu na Babbi walikutana tena jana Uwanja wa UiTM mjini Shah Alam, Malaysia katika mchezo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo.
  Babbi aliiongoza timu yake, Universiti Teknologi MARA (UiTM) kuifunga Sabah ya Diouf mabao 2-1 na vizuri zaidi wawili hao kila mmoja aliifungia timu yake.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY kutoka Malaysia leo, Babbi alisema; “Tumecheza dhidi ya timu ya akina Diouf, tukashinda 2-1, mimi nilifunga bao moja la timu yetu, na Diuof aliifungia timu yake kwa penalti,”.
  Pamoja na hayo, Babbi akasema licha ya kufurahi kulipa kisasi cha mwaka 2007, lakini amefurahi pia Diouf alimkumbuka jana. “Jamaa amenikumbuka na tulizungumza uwanjani, huenda leo jioni akanipigia simu tukakutana naye,”amesema Babbi.   
  Diouf baada ya kuwika Ulaya katika klabu za Sochaux, Rennes na Lens zote Ufaransa, Liverpool, Bolton Wanderers, Sunderland and Blackburn Rovers za England, Rangers na Doncaster Rovers za Scotland, kwa sasa anamalizia soka yake Malaysia. 
  Katika kipindi cha miaka yake tisa ya kuichezea Senegal ikiwemo kuifikisha Robo Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2007, Diouf amewafungia Simba wa Teranga mabao 21 katika mechi 69.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ABDI KASSIM ‘BABBI’ ALIPA KISASI KWA DIOUF, AMTANDIKA 2-1 MALAYSIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top