• HABARI MPYA

  Jumamosi, Februari 28, 2015

  SIMBA SC YAFANYA MAUWAJI HAIJATOKEA MSIMU HUU, YAITANDIKA PRISONS 5-0 TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imezinduka kutoka kwenye kipigo cha 1-0 cha Stand United wiki iliyopita mjini na Shinyanga na jioni ya leo kuitandika mabao 5-0 Prisons ya Mbeya.
  Kwa ushindi huo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba SC sasa inatimiza pointi 23, baada ya mechi 16, ingawa inabaki nafasi ya nne nyuma ya Kagera Sugar yenye pointi 24, Azam FC pointi 27 na Yanga SC 31.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo wa Mara, hadi mapumziko, tayari Simba SC ilikuwa mbele kwa mabao 3-0, yote yakifungwa na mshambuliaji chipukizi, Ibrahim Salum Hajibu.
  Ibrahim Hajibu akishangilia baada ya kukamilisha hat trick yake leo dhidi ya Prisons Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

  Hajibu alifunga bao la kwanza dakika ya 15 akimalizia pasi nzuri ya Mganda, Dan Sserunkuma ambaye alimlamba chenga beki wa Prisons Nurdin Chona kabla ya kumpasia mfungaji aliyemchambua kipa Mohammed Yussuf.
  Bao la pili Hajibu alifunga dakika ya 21 akimalizia mpira uliotemwa na kipa kipa Mohammed Yussuf, kufuatia shuti la mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi.
  Hajibu alikaribia kukamilisha hat tric mapema dakika ya 24 baada ya kupiga vizuri mpira wa adhabu uliokoolewa na kipa Mohammed Yussuf na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
  Lakini mchezaji huyo zao la Simba B, akatimiza ndoto zake za hat trick dakika ya 41 baada ya kufunga kwa penalti, kufuatia beki wa Prisons Lugano Mwangama kuunawa mpira kwenye eneo la hatari. 
  Kwa ujumla Simba SC, ikiongozwa na viungo ‘mafundi’ Jonas Mkude na Said Ndemla ilitawala kipindi cha kwanza, wakati Prisons ilifanya mashambulizi kadhaa ya kushitukiza kupitia pembeni, ambayo yalizimwa na ngome ya Wekundu wa msimbazi.
  Mshambuliaji wa SImba SC, Mganda Dan Sserunkuma akipambana na beki wa Prisons, Nurdin Chona kulia
  Mfungaji wa mabao matatu ya Simba SC, Ibrahim Hajibu akimtoka Nurdin Chona wa Prisons kabla ya kufunga bao la pili
  Hajibu akiwapungia mashabiki wa SImba SC baada ya kuwapa 'roho zao zinapenda'. Kulia ni Messi aliyefunga bao la tano na kushoto Sserunkuma

  Kipindi cha pili, Simba SC waliendelea kutawala mchezo na kupata mabao mawili zaidi, yaliyofungwa na Mganda Emmanuel Okwi na mzalendo Ramadhani SIngano ‘Messi’.
  Okwi alianza kufunga dakika ya 75 akifumua shuti kali baada ya kupokea pasi ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Messi akakamilisha dakika ya 84 akimalizia krosi ya Okwi.
  Awali, dakika ya 68 Nurdin Chona wa Prisons alitolewa nje kwa kadi ya pili ya njano baada ya kumtolea maneno machafu refa Adongo. 
  Simba SC; Ivo Mapunda, Hassan Kessy/Nassor Masoud ‘Chollo’ dk61, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’, Said Ndemla, Dan Sserunkuma/Twaha Ibrahim ‘Messi’ dk76, Ibrahim Hajib/Awadh Juma dk67 na Emmanuel Okwi.
  Prisons; Mohammed Yussuf, Lugano Mwangama, Laurian Mpalile, James Mwasote, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil/John Mathei dk34, Adam Chimbongwe/Meshack Suleiman dk50, Freddy Chudu, Ibrahim Isaka, Boniface Hau/Julius Kwanga dk46 na Godfrey Magetha.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAFANYA MAUWAJI HAIJATOKEA MSIMU HUU, YAITANDIKA PRISONS 5-0 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top