• HABARI MPYA

    Thursday, February 19, 2015

    DIDIER KAVUMBANGU: MSHAMBULIAJI UNAYEHITAJI KUWA NAYE KATIKA KIKOSI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    AKIWA katikati ya msimu wake wa kwanza katika klabu ya Azam FC, tayari mshambuliaji Mrundi, Didier Kavumbangu amefikisha nusu ya mabao aliyofunga ndani ya misimu yake miwili Yanga SC.
    Yanga SC ndio waliomleta Tanzania mshambuliaji huyo mrefu mwaka 2012, baada ya kuvutiwa naye kufuatia kumuona katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mjini Dar es Salaam akiwa na klabu ya Atletico ya kwao.
    Na katika mechi ya makundi akiwa na jezi ya Atletico, baada ya kuwafunga mara mbili Yanga SC, Kavumbangu ‘aliwaloga’ kabisa wana Jangwani na kuingia msituni kuisaka saini yake.
    Didier Kavumbangu amefikisha mabao 14 katika mechi 27 Azam FC
    Kavumbangu alifunga mabao 31 katika mechi 63 ndani ya misimu miwili Yanga SC

    Hatimaye akasajiliwa kwa ajili ya msimu wa Ligi Kuu 2012/2013 na mwisho wa msimu akaiwezesha timu hiyo kurejesha taji la ligi hiyo kutoka kwa mahasimu, Simba SC.
    Yanga SC ikazidiwa kete na Azam FC msimu wa 2013/2014 katika vita ya taji la Ligi Kuu na wakati huo Kavumbangu tayari amemaliza Mkataba wake Jangwani akiwa amecheza mechi 63 na kufunga mabao 31, moja tu la penalti. 
    Kwa wastani huu wa mabao unataka nini zaidi kwa mshambuliaji? Lakini ajabu Yanga SC wakazembea kumsainisha Mkataba mpya na mchezaji huyo akaibukia Azam FC ambako hadi sasa amecheza mechi 27 na kufunga mabao 14.
    Mabao 14 tayari ni karibu nusu ya mabao aliyofunga Yanga SC ndani ya mechi 63 za misimu miwili- maana yake moto wa Kavumbangu unazidi kukolea.  
    Mchezaji ambaye anaonekana kuwa na makali ya kutishia ufalme wa mabao wa Kavumbangu ni Mrundi mwenzake, Amissi Tambwe. 
    Tambwe alifunga mabao  26 katika mechi 43 za msimu mmoja na nusu Simba SC, pia akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita na baada ya kutua Yanga SC Desemba mwaka jana, hadi sasa amecheza 10 na kufunga mabao matatu, moja la penalti.
    Mjfungaji bora wa Kenya misimu miwili mfululizo iliyopita akiwa na Gor Mahia, Dan Sserunkuma baada ya kutua Simba Desemba pia, hadi sasa amefunga mabao matano katika mechi 12. 
    Mfungaji bora wa zamani wa Liberia na Cyprus Kaskazini, Kpha Sherman aliyetua Yanga SC Desemba pia, amefunga mabao mawili katika mechi 12.
    Winga Brian Majwega aliyesajiliwa Azam FC Desemba pia kutoka KCCA ya kwao, Uganda amecheza mechi 13 bila kufunga, lakini amekuwa mpishi mzuri wa mabao na tegemeo la timu yake mpya.
    Hapa unaweza kuona Didier Kavumbangu ni aina ya mshambuliaji ambaye unapaswa kuwa naye katika timu. Ana uchu wa mabao na ni mfungaji wa uhakika, si wa kubahatisha.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DIDIER KAVUMBANGU: MSHAMBULIAJI UNAYEHITAJI KUWA NAYE KATIKA KIKOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top