• HABARI MPYA

    Wednesday, February 18, 2015

    KILI MARATHON 2015, MGENI RASMI WAZIRI CHIKAWE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Mhe. Mathias Chikawe atakuwa mgeni rasmi kwenye mbio za 13 za Kilimanjaro Marathon zinazotarajiwa kufanyika Jumapili tarehe 1 Machi, 2015 huko Moshi.
    Aggrey Marealle, Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions, waratibu wa mbio hizo alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa Waziri Chikawe  ataanzisha mbio hizo zinazotarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 6,000 kutoka nchi zaidi ya 40 na atakuwa mgeni rasmi katika sherehe ya kutoa zawadi ambapo atatoa zawadi kwa washindi 10 wa mbio za 42km Kilimanjaro Premium Lager Marathon.

    Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Mathias Chikawe atakuwa mgeni rasmi kwenye mbio za 13 za Kilimanjaro Marathon 

    “Mhe. Chikawe amekubali kuanzisha mbio na kutoa zawadi kwa washindi wa 42km Kilimanjaro Premium Lager Marathon kwa wanaume na wanawake,” alisema Marealle. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Leonidas Gama atakuwa ni kati ya wageni mashuhuri watakaohudhuria tukio hilo.
    Marealle aliongeza kuwa Kilimanjaro Marathon ni tukio ambalo limeendelea kuongeza  hadhi ya Tanzania kimataifa kila mwaka; na imesaidia kutambua na kutoa fursa kwa wanariadha wa ndani kukua zaidi, kukuza utalii wa Tanzania na watu kupata nafasi ya kufurahi zaidi.
    Alisema mbio hizo zitakuwa na viwango vya kimataifa kama ilivyo kawaida na zitasimamiwa na Kilimanjaro Marathon Club, Riadha Tanzania na Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro. Ili kuhakikisha usalama wa wanariadha na washiriki wote kwa ujumla, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imetoa kibali cha kufungwa kwa baadhi ya barabara za ndani na nje ya mji wa Moshi ambazo zitatangazwa badae zitafungwa kwa muda saa 12:15 asubuhi hadi 02:00 asubuhi tarehe 1, Machi 20135ili kuruhusu waanariadha kupita salama kwani mbio hizi zimekuwa na ongezeko kubwa la washiriki kila mwaka jambo ambalo linalazimu waandaaji kuimarisha usalama.
    Marealle alisema kuwa “Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chao cha Kilimanjaro Premium Lager ndio wadhamini wakuu wa Kilimanjaro Marathon na shughuli zingine za burudani baada ya riadha, na wamekuwa wadhamini wa tukio hili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003. Juhudi zao katika masoko na matangazo imekuwa mchango mkubwa katika kukuza mbio hizi. Nawaomba wananchi wa Moshi na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki na kushangilia watakaoshiriki kwani kuna kuna zawadi za kuvutia kutoka kwa wadhamini pamoja na medali na fedha taslimu kwa washindi ”.
    Marealle alisema kuwa mbio hizi zimejipatia umaarufu mkubwa kutokana na kuungwa mkono na wananchi wa Moshi na vilevile kuungwa mkono na serikali ya mkoa pamoja na taasisi kama polisi na manispaa ya Moshi. 
    Mbio hizo zinaratibiwa na Executive Solutions kwa kushirikiana na Riadha Tanzania, Chama cha Riadha Kilimanjaro na Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na wadhamini wakuu Kilimanjaro Premium Lager, Tigo (Tigo Kili Half Marathon), GAPCO (Walemavu), Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar,  CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, Kibo Palace Hotel, UNFPA na Kilimanjaro Water.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILI MARATHON 2015, MGENI RASMI WAZIRI CHIKAWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top