• HABARI MPYA

    Wednesday, February 25, 2015

    HII NDIYO SILAHA BORA KWA AZAM FC, YANGA SC MECHI ZA UGENINI AFRIKA

    WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Afrika, Azam FC na Yanga SC wanaelekea ugenini kwa mechi za marudiano Raundi ya Awali.
    Azam FC waliondoka jana usiku kwenda Sudan, kumenyana na El Merreikh katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Yanga SC wanaondoka asubuhi ya leo kwenda Botswana kwa mchezo wa marudiano na BDF XI ya Botswana katika mchezo wa marudiano Raundi ya Awali, Kombe la Shirikisho Afrika.
    Vyema timu zote zilianza na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani, Azam Uwanja wao wa Azam Complex na Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

    Ushindi wa mabao 2-0 si hazina mbaya kuelekea michezo ya marudiano ugenini kwa wawakilishi wetu hao.
    Pamoja na hayo, Azam FC na Yanga SC wanapaswa kutambua kwamba kama walioshinda 2-0 nyumbani, basi na wapinzani wao wanaweza kupata ushindi wa aina hiyo, au zaidi wakiwa nyumbani.
    Timu zote mbili zilipoteza nafasi zisizopungua tatu kila timu za kufunga mabao zaidi. Zilikuwa nafasi za wazi, lakini ndiyo soka- bora zilishinda.
    Ni imani yangu kwamba, makocha wa timu hizo, Mcameroon Joseph Marius Omog wa Azam FC, anayesaidiwa na Mganda, George ‘Best’ Nsimbe na Mholanzi, Hans van der Pluijm wa Yanga SC anayesaidiwa na mzalendo, Charles Boniface Mkwasa watakuwa wamefanyia kazi mapungufu baada ya mechi za awali.
    Na kubwa lilikuwa katika umakini wa kutumia nafasi- tumeona Yanga SC katika mechi zao mbili za Ligi Kuu wamefunga mabao sita na kufungwa moja.
    Maana yake, wamejirekebisha kidogo katika utumiaji nafasi, hasa ikizingatiwa walicheza ugenini dhidi ya timu ngumu, Prisons (3-0) na Mbeya City (3-1).
    Lakini Azam FC hawajashinda hata bao moja katika mechi zao mbili za Ligi Kuu, wakitoa sare za 0-0 na Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani na Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
    Inawezekana mipango ya mechi ya marudiano dhidi ya Merreikh ilichangia matokeo ya sare katika mechi mbili za Azam FC Ligi Kuu.
    Dalili zilionekana katika mechi zote, wachezaji wa Azam FC walicheza kwa tahadhari ya kuepuka kuumia, na matokeo yake hawakujitoa kwa asilimia 100 uwanjani- haikushangaza sana walipata sare.
    Naamini juu ya mipango ya walimu wa timu zote mbili kuelekea michezo ya marudiano, lakini si vibaya nikatumia fursa hii kuwasistiza umuhimu wa kwenda kuulinda ushindi wao ugenini.
    Zote, Azam FC na Yanga SC zinapaswa kwenda kucheza kwa kushambulia katika mechi za marudiano badala ya kufikiria kwenda kujilinda.
    Njia nzuri ya kujilinda ni kushambulia, ili kuepuka kushambuliwa wewe- na kama Azam FC na Yanga watakwenda kufanya hivyo katika mechi zao mwishoni mwa wiki, watafanikiwa.
    Wakithubutu kwenda kucheza kwenye eneo lao, watawakaribisha wapinzani ambao watakuwa wanashangiliwa na maelfu ya mashabiki wa nyumbani, matokeo yake kujihatarisha kufungwa.
    Na kwa tathmini ya baada ya mechi za awali, wazi wote Yanga SC na Azam FC wana nafasi ya kwenda kushinda na ugenini pia, iwapo wataweka dhamira hiyo.
    Tunafahamu mpira wa Afrika una matatizo yake, vile vitu vinaitwa hujuma na hila chafu zisizo za kiuanamichezo wote Yanga SC na Azam FC wavitarajie katika mechi za ugenini.
    Kwa Azam FC ndiyo wanakwenda kwenye vita kweli, kwa sababu hiyo ndiyo hulka ya timu za Sudan miaka nenda, rudi. Azam FC wajue wanakwenda kupambana na wanatakiwa wawe wamejipanga kwa vita ya ndani na nje ya Uwanja.
    Zaidi ya hayo, niwatakie safari njema wawakilishi wetu hao- lakini kubwa tu ni kwamba, wanapaswa kwenda kushambulia ugenini, ili kujiepusha kushambuliwa wao na kukaribisha kufungwa. Kila la heri Azam na Yanga SC, ila silaha nzuri ya kuyalinda matokeo yao ya awali ni kushambulia ugenini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HII NDIYO SILAHA BORA KWA AZAM FC, YANGA SC MECHI ZA UGENINI AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top