• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 19, 2015

  LIGI MBILI KENYA!!! NGOMA NGUMU NA KALI HII

  Na Vincent Malouda, NAIROBI
  TAIFA la Kenya kwanzia ino wikiendi litashuhudia ligi mbili zikiendeshwa na vyama viwili tofauti.
  Shirikisho la Soka la Kenya, FKF, limesema ligi yao ya timu 18 itaendelea wikiendi hii baada ya kutoafikiana na Kampuni inayosimamia ligi kuu, KPL, kwenye mkutano wa kujaribu kutafuta suluhisho uliyofanyika jana ilivyoagizwa na katibu katika wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni, Daktari Hassan Wario siku ya Jumatatu alipokutana na maafisa wa FKF na KPL.
  Katika mkutano huo, Waziri Wario aliviagiza vyama hivyo viwili kuweka malumbano yao kando na kuelewana kabla ya siku ya jumatano, yaani hivi leo la sivyo achukue sheria mikononi, jambo ambalo wameshindwa kutimiza hivo kutangaza kuwa ligi zao zitaendelea.

  “Ligi itaanza ino wikiendi kama ilivyoratibiwa hapo awali. Tumekosa kuelewana jinsi waziri alivyoagiza kwa sababu shirikisho chini ya rais wake Sam Nyamweya lilitaka tupige kura lakini hao walikuwa wengi manake waliwaita wanachama wa matawi yao nchini kutuzidi sisi hivo wao wangeshinda kwa idadi,” alisema mwenyekiti wa kampuni inayosimamia ligi kuu, KPL, bwana Ambrose Rachier ambaye pia ni mwenyekiti wa Gor Mahia.
  Kwa upande wake, Rais Nyamweya alivionya vilabu vyovyote vitakavyoshiriki katika ligi isiyotambulika na shirikisho huku waamuzi watakaosimamia mechi hizo wakipigwa marufuku.
  “Timu zote zina hadi kesho (Alhamisi) saa kumi asubuhi kuthibitisha kuwa watashiriki ligi itakayoendeshwa na shirikisho la sivyo nafasi zao zitachukuliwa na vilabu vingine ambavyo vimeeleza nia ya kucheza ligi yetu,” Nyamweya alifoka katika mahojiano na wanahabari waliyokita kibanda nje ya mkutano huo, BIN ZUBEIRY ikiwemo.
  Klabu kumi na sita zilizoshiriki ligi kuu msimu jana tayari zimetangaza msimamo wao wa kutoshiriki ligi isiyokuwa na mfadhili na inayoendeshwa na watu waliyoweka matumbo yao mbele kwa maana ya FKF.
  SuperSport International ya Afrika Kusini ambayo ina haki ya kuzionyesha mechi za Kenya na kampuni ya vileo, Tusker, pia wamesalia na msimamo wao wa kufadhili ligi yenye timu 16 na sio 18 anavyotaka Nyamweya.
  Mwishoni mwa wiki jana, Shirikisho la Soka duniani, FIFA, lilizionya FKF na KPL kuwa huenda zikapigwa marufuku iwapo watakosa kupata muafaka unaowafaa wakenya. Basi kilichosalia sasa ni aidha serikali itoe uamuzi wake au FIFA iingilie kati.
  Tayari ligi ya FKF ilishang’oa nanga wikiendi iliyopita Shabana FC wakimzaba Nakumatt FC 1 – 0 uwanjani Machakos katika mechi ya kwanza huku ya KPL ikitarajiwa kuanza wikiendi hii.
  SuperSport huzipa kila klabu shilingi za Kenya milioni 7.5 kwa msimu huku bingwa akipata shilingi za Kenya milioni 4.5. FKF kufikia sasa haijazindua mfadhili wao jambo linalozitia hofu klabu kutoshiriki ligi hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: LIGI MBILI KENYA!!! NGOMA NGUMU NA KALI HII Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top