• HABARI MPYA

    Sunday, February 01, 2015

    INAPOFIKIA MASHABIKI WANAWAPELEKA PUTA VIONGOZI, BASI NI HATARI

    KATIKATI ya wiki nilizungumzia mapungufu ya viongozi wetu wa klabu siku hizi na nikaelezea umuhimu wa watu hao kubadilika.
    Huo ulikuwa upande mmoja tu wa matatizo ya soka yetu, lakini ukweli ulivyo ni kwamba soka yetu inaogelea kwenye bwawa la matatizo makubwa.
    Na kubwa ambalo linaonekana kukua kwa kasi katika siku za karibuni ni viongozi wa klabu kuyumbishwa na mashabiki, kiasi cha kufikia kufanya maamuzi ya kuvuruga timu.
    Maamuzi mengi ndani ya Simba SC na Yanga SC hususan ya kuvunja mabenchi ya ufundi au kufukuza wachezaji, huwa hayatokani na hali halisi, bali presha za mashabiki.
    Viongozi wameshindwa kabisa kumudu presha za mashabiki na matokeo yake wamekuwa wakivuruga zaidi mambo katika klabu.

    Inapotokea timu ikapoteza mechi, mashabiki wakipiga kelele kidogo tu, utasikia timu imesimamisha wachezaji, imefukuza kocha.
    Na hatua kama hizo ndizo hutuliza presha ya mashabiki- na imeendelea kuwa desturi kiasi kwamba inachangia hata kuzorotesha maendeleo ya klabu.
    Hapa zinazungumziwa klabu kongwe, Simba na Yanga SC ndizo ambazo katika miaka ya karibuni zimekosa bahati ya kupata viongozi wastahmilifu, wenye uwezo wa kumudu presha ya mashabiki.
    Sasa wapo mashabiki wanajiona wao ni mabosi wa viongozi na wamejijengea urafiki na watangazaji wa Redio, timu ikiteleza kidogo tu, anapewa nafasi anakashifu viongozi na kuwatisha waondoke madarakani.
    Kwa presha, viongozi wanachukua hatua nyingine za kuwaonea tu wachezaji na makocha ili mradi wajisafishe wao mbele ya wapenzi wa timu, pasipo kuzingatia anaiathiri kiasi gani timu.
    Kwa nini kocha Mholanzi Ernie Brandts alifukuzwa Yanga SC? Ni baada ya kufungwa na Simba SC katika mechi ya Nani Jembe Desemba mwaka juzi mabao 3-1.
    Lakini tunashuhudia timu kubwa Ulaya, mfano England pale bingwa wa Ligi Kuu na timu yenye kikosi ghali zaidi, Manchester City anatolewa kwenye mashindano ya FA na timu ya Daraja la Kwanza- wala hakuna shida, maisha yanaendelea.
    Huku kwetu hali ni tofauti sana na kwa kweli ni vigumu mno kufanya kazi Simba au Yanga SC, ikiwa viongozi wanaweza kuchukua maamuzi yoyote kwa presha ya mashabiki.
    Wakati umefika sasa, viongozi wa Simba na Yanga SC wabadilike- wawe na ujasiri wa kuweza kukabiliana na presha za mashabiki, ili kuwarahisishia kazi makocha na wachezaji.
    Nimekuwa nikimfuatilia kocha mpya wa Simba SC, Mserbia Goran Kopunovic tangu ameanza kazi Msimbazi kwa kweli amekuwa hana furaha ya moja kwa moja, japokuwa alianza vizuri akiipa timu Kombe la Mapinduzi.
    Hana raha kwa sababu anajua desturi na historia ya Simba SC, kwamba imekuwa ‘si timu ya mpira’ siku hizi bali ni timu ya ‘Kiswahili Swahili tu’.
    Anajua wakati wowote atawekewa mizigo yake nje ya chumba cha hoteli anayoishi ili arejee kwao. Tafakari huyo mtu anaweza kufanya kazi kwa ufanisi wa kutosha?
    Tunaona, kila siku kiwango cha Simba SC na wachezaji kinashuka badala ya kupanda, kwa sababu hakuna mwenye furaha na kazi kati yao. Wote hawajiamini. Ufanisi utoke wapi?
    Ramadhani Singano ‘Messi’ anajua sababu zilizomfanya Haroun Chanongo akatolewa kwa mkopo Stand United, hivyo anapoanza kusikia ‘maneno maneno’ yanaanza juu yake, basi atahisi tu anafuata nyayo za mwenzake waliyeibuka naye pamoja timu ya vijana ya klabu.
    Kwa kweli huu si utaratibu kabisa, Rais wa Simba SC, Evans Aveva na Kamati yake ya Utendaji lazima waonyeshe ukomavu. Lazima wamaanishe ule ‘utoto wa mjini’ wao kwa kutokubali kuyumbishwa na mashabiki.
    Rais aliyetangulia, Alhaj Ismail Aden Rage aliweza kumudu presha ya mashabiki na vikundi vyote alipokuwa madarakani, tatizo moja tu, hakupata sapoti ya wadau wengine wa klabu, hata iwe kwa tabia zake mwenyewe kuwakera wengine.
    Rage alionyesha kwamba ni mtoto wa mjini haswa na anazijua vyema siasa za Simba na Yanga na hata wapinzani wake ilifika wakati wakasalimu amri na kumuacha amalize muda wake madarakani.
    Mimi najua Rage atakuwa anawacheka sana hawa mabwana walio madarakani hivi sasa Simba SC, kwa sababu ‘wanatokoteshwa’ na mashabiki hadi wanafanya maamuzi ya kuivuruga timu.
    Ilivyo sasa, Simba SC inahitaji kutulia na mwalimu mmoja, amalize msimu na aanze maandalizi ya msimu mpya kwa kusajili timu mwenyewe.
    Lakini kama kocha atakuwa anafanya kazi bila kujiamini, saa ngapi atafikiria namna ya kuboresha timu kwa ajili ya msimu unaofuata? 
    Kwa kweli, inapofikia mashabiki wanawapeleka puta viongozi wa klabu, ni hatari sana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: INAPOFIKIA MASHABIKI WANAWAPELEKA PUTA VIONGOZI, BASI NI HATARI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top