Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
VIGOGO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam FC, Mtibwa Sugar, Simba na mahasimu wao, Yanga SC wamekwenda wote Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, huku kukiwa kuna uwezekano wa kukutana baina yao katika Nusu Fainali.
Robo Fainali ya kwanza itachezwa kesho Saa 2:15 Usiku Uwanja wa Amaan, kati ya Simba SC na Taifa ya Jang’ombe, wakati keshokutwa Yanga SC itamenyana na JKU, mchezo ambao utatanguliwa na mechi kati ya KCCA na Polisi Saa 9:00 Alasiri, Azam FC na Mtibwa Sugar Saa 11:00.
Simba SC inaweza kukutana na KCCA ya Uganda katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapindzi Januari 10, mwaka huu
Kwa mujibu wa Ratiba ya mashindano haya, Nusu Fainali zitachezwa Januari 10 Uwanja wa Amaan, ambazo zitawakutanisha mshindi kati ya Simba na Taifa dhidi ya mshindi kati ya KCCA ya Uganda na Polisi Zanzibar na mshindi kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar dhidi ya mshindi kati ya Yanga na JKU.
Simba SC inapewa nafasi kubwa ya kuitoa Taifa na KCCA inapewa nafasi kubwa ya kuitoa Polisi- hivyo kuna uwezekano timu hizo zilizokutana katika Fainali mwaka jana, zikakutana katika Nusu Fainali mwaka huu.
Yanga SC inapewa nafasi ya kuitoa JKU, wakati mchezo kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar, lolote linaweza kutokea.
Kwa vyovyote, uhondo wa Kombe la Mapinduzi unaanza kesho wakati wa Robo Fainali, Simba SC ikimenyana na Taifa, ambayo walikutana nayo katika mchezo wa kirafiki na kushinda 3-1 Uwanja wa Amaan.
Hatua ya makundi ya michuano hiyo imefikia tamati leo mchezo wa mwisho wa Kundi A, kati ya Yanga SC na Shaba Uwanja wa Amaan usiku huu. Yanga SC, imeshinda 1-0 bao pekee la winga Mbrazil, Andrey Coutinho dakika ya 86.
0 comments:
Post a Comment