• HABARI MPYA

    Saturday, October 04, 2014

    SIMBA SC HALI TETE, YATOA SARE TENA NA STAND LICHA YA KUONGOZA KWA BAO ZURI LA KISIGA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imelazimishwa sare ya tatu mfululizo nyumbani leo, baada ya kufungana bao 1-1 na Stand United ya Shinyanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Simba SC kama ilivyokuwa katika mechi zake mbili za awali, zote iliongoza 2-0 na Coastal ikaisha 2-2 na 1-0 na Polisi Moro ikaisha 1-1 na leo pia iliongoza ‘ikachomolewa’. 
    Hadi mapumziko, tayari timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Simba SC wakitangulia kupitia kwa Shaaban Kisiga ‘Malone’ dakika ya 35 kabla ya Stand kusawazisha dakika 10 baadaye.
    Kisiga alifunga bao bora la mechi ambalo mwisho wa msimu linaweza kuingia kwenye orodha ya mabao bora ya Ligi Kuu, baada ya kupokea pasi ya Mganda Emmanuel Okwi na kupangua ukuta wa Stand na kipa wao, kisha kusukuma gozi nyavuni.
    Kiungo wa Simba SC, Shaaban Kisiga 'Malone' akimtoka beki wa Stand United, Reyna Mgungira
    Emanuel Okwi kushoto na Ibrahim Hajib kulia wakimpongeza Kisiga baada ya kufunga

    Baada ya bao hilo, Simba SC iliongeza kasi ya mashambulizi, lakini ukuta wa Stand ukiongozwa na beki wa zamani wa Azam FC, Omar Mtaki ulikuwa imara kudhibiti vishindo hivyo.
    Stand walifanikiwa kusawazisha dakika ya 45 kwa shambulizi la kushitukiza wakitoka kushambuliwa- kupitia kwa Kheri Mohammed aliyepokea pasi ya Mganda Suleiman Jingo na kumchambua kipa Hussein Sharrif ‘Cassilas’.
    Kipindi cha pili, kocha wa Simba SC, Mzambia  Patrick Phiri alianza na mabadiliko akimpumzisha winga Ramadhani Singano ‘Messi’ na kumuingiza kiungo Said Ndemla.
    Mabadiliko hayo yaliisaidia Simba SC kuongeza mashambulizi langoni mwa Stand, lakini hata hivyo, Wekundu wa Msimbazi waliishia kupoteza nafasi walizotengeneza za kufunga.
    Stand waliendelea kushambulia kwa kushitukiza na kulitia misukosuko lango la Simba SC mara mbili kipindi hicho cha pili.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Hussein Sharrif ‘Cassilas’, Miraj Adam, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Joram Mgeveke, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’/Said Ndemla dk46, Shaaban Kisiga ‘Malone’/Amri Kiemba dk84, Emmanuel Okwi na Ibrahim Hajibu/Elias Maguri dk68.
    Stand United; John Mwenda, Swaleh Abdallah, Yassin Mustafa, Iddi Mobby, Peter Mutabuzi, Omar Mtaki, Mussa Said, Reyna Mungira, Kheri Mohamed, Soud Mohammed/Salum Kamana dk70 na Suleiman Jingo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC HALI TETE, YATOA SARE TENA NA STAND LICHA YA KUONGOZA KWA BAO ZURI LA KISIGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top