• HABARI MPYA

    Monday, April 01, 2013

    MSIBA, MSIBA SOKA TANZANIA, WANASOKA WAWILI WAAGA DUNIA TANGA NA TABORA

    Haruna Moshi 'Boban'; Mmoja wa wanasoka mahiri kutoka mkoani Tabora ambako kuna msiba mzito hivi sasa baada ya kifo cha mchezaji wa Polisi. 

    Na Mwandishi Wetu
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mshambuliaji wa timu ya Ligi Daraja la Kwanza Bara (FDL), Polisi Tabora, Regan Mbuta kilichotokea jana (Machi 31 mwaka huu) usiku kwa ajali ya pikipiki mjini Tabora.
    Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tabora (TAREFA), Yussuf Kitumbo, marehemu anatarajiwa kusafirishwa leo (Aprili 1 mwaka huu) kwenda kijijini kwao Kimamba, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kwa ajili ya mazishi.
    Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema kwamba msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu, kwani Mbuta alikuwa mmoja wa washambuliaji tegemeo wa Polisi Tabora, na bao lake la mwisho aliyoifungia timu ilikuwa kwenye mechi ya mwisho ya FDL msimu huu dhidi ya Pamba ya Mwanza iliyochezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
    Wambura amesema TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mbuta, TAREFA na klabu ya Polisi Tabora na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito, huku akiomuombea marehemu; Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amina.
    Aidha, TFF pia imesema imepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Coastal Union ya Tanga, TPC na Taifa Stars, Behewa Ali Sembwana aliyekuwa na umri wa miaka 72, kilichotokea jana usiku (Machi 31 mwaka huu) mkoani Tanga.
    Wambura amesema msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Sembwana akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea, hivyo mchango wake utakumbukwa daima.
    Sembwana aliyekuwa akicheza wingi ya kulia alidumu katika Taifa Stars kwa miaka 10, kama ilivyokuwa kwa kombaini ya Mkoa wa Tanga (Tanga Stars) aliyoiwakilisha katika michuano ya Kombe la Taifa, Taifa Cup alikuwa hodari enzi zake.
    Wambura amesema TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Sembwana, Chama cha Soka Tanga (TRFA) na klabu ya Coastal Union na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
    Amesema mazishi ya marehemu Sembwana yanatarajiwa kufanyika leo (Aprili 1 mwaka huu) kijijini kwake Lusanga, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga. Mungu aiweke roho ya marehemu Sembwana mahali pema peponi. Amina.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MSIBA, MSIBA SOKA TANZANIA, WANASOKA WAWILI WAAGA DUNIA TANGA NA TABORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top