![]() |
| Rebecca Malope mmoja wa nyota waliotumbuiza tamasha la Pasaka |
KAMPUNI ya Msama Promotions,
waandaaji wa tamasha la Pasaka, inatarajia kuanza kutekeleza ahadi yake ya
kuwasaidia wanawake wajane na watu wasiojiweza fedha za mitaji ya biashara.
Mkurugenzi wa Msama Promotions,
Alex Msama, alisema kwa njia ya simu jana kutoka Dodoma kuwa Kamati ya
Maandalizi ya Pasaka inatarajia kwenda Mtwara Jumatatu kufanya tathmini ya
maeneo ya kutoa msaada.
"Kamati inatarajia kwenda
Mtwara Jumatatu kufanya tathmini ya maeneo gani ya kusaidia wasiojiweza...
safari hii walengwa hasa ni watu wa vijijini.
"Kama ilivyo ada, kamati
yetu haitoa msaada kwa kubagua itikadi za kidini, awe Mkirsto au Muislamu, wote
tunawapa msaada na ndiyo maana hata Serikali imekuwa mstari wa mbele kutuunga
mkono.
"Tunasaidia wasiojiweza
wote wakiwamo wanawake wajane, watoto yatima na walemavu bila kujali udini...
watu wa imani zote za dini tunawatendea haki kwa vile hata kwenye matamasha ya
Pasaka, wanaohudhuria ni watu wa imani zote za dini," alisema Msama.
Alisema wamekusudia kutimiza
ahadi waliyoitoa wakati wa maandalizi ya tamasha la Pasaka lililofanyika Aprili
8 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na lile la Jumatatu ya Pasaka,
Aprili 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Msama juzi alitoa taarifa ya
kuwashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha tamasha hilo kwa hali na mali.
Katika tamasha la Uwanja wa
Taifa, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, ambaye pamoja na marafiki zake alioongozana nao jukwaani
walichangia sh. milioni 10, Rais Kikwete aliahidi kuchangia sh. milioni 10 na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda sh. milioni 5, hivyo kufanya jumla kuwa sh. milioni
25, zitakakazotumika kusaidia wasiojiweza.
Pia katika tamasha la Dodoma,
Naibu Spika, Job Ndugai alichangia sh. milioni 2 kwenye mfuko huo.
Mwaka jana, wanawake wajane
waliokabidhiwa fedha za mitaji walitoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na
Morogoro ambapo sh. milioni 4 zilitumika. Fedha nyingine zilitumika kusaidia
kusomesha watoto yatima.



.png)
0 comments:
Post a Comment