• HABARI MPYA

  Monday, April 30, 2012

  NINI HASWA KIMEMFANYA PEP GUARDIOLA AACHIE NGAZI BARCA?


  Barca wakifuatia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita Uwanja wa Wembley, chini ya kocha Guardiola

  UNADHANI nini kimemwondoa Pep Guardiola Barcelona? Je, aliona kutosheka baada ya kutumia vizuri muda wake alipokuwa Catalan? Je, ni sahihi kwa kipindi hiki alichoondoka na kuiacha timu mikono mitupu?
  Jibu la waliowengi watasema kwamba kukosa nafasi ya kunyakua taji lolote kwa msimu huu – ndicho chanzo kikubwa kilichofungua njia kwa kocha huyo kuamua kufungasha virago vyake.
  Guardiola alishuhudia kikosi chake kikipoteza nafasi ya kutetea ubingwa wa La Liga mbele ya Real Madrid baada ya kunyukwa kwenye mechi ya El Clasico.
  Na mbaya zaidi, siku chache baadaye, wababe hao wa Nou Camp walijikuta wakilitema taji jingine la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baada ya kutupwa nje ya michuano hiyo katika hatua ya nusu fainali na Chelsea.
  Lakini, kuna jambo ambalo mashabiki wa soka watakuwa hawalifahamu lililomfanya Guardiola kuamua kusahau mafanikio yake aliyopata kwenye kikosi hicho katika misimu yake minne aliyodumu na kuamua kuondoka.
  Pep ameamua kung’atuka Barca mwishoni mwa msimu huu kwasababu ya tofauti zake zilizoibuka dhidi ya rais wa klabu na presha inayowakabili wachezaji wake.
  Oktoba mwaka jana – mchambuzi wa masuala ya michezo, Antony Kastrinakis – anayeandika kolamu yake ya Kastro kwenye gazeti la The Sun, aliwaeleza wasomaji wake kwamba Guardiola atang’atuka Barca mwishoni mwa msimu.
  Na hilo kwa kiasi kikubwa lilichangiwa na hasira zilizopo baina ya rais Sandro Rosell dhidi ya mtangulizi wake, Joan Laporta.
  Na hilo lilithibitishwa kama alivyozungumza Guardiola mwenyewe kwamba: “Nilimweleza rais mwisho mwa Septemba au mwanzoni mwa Oktoba kwamba huu ni msimu wangu wa mwisho.”
  Kwa kauli hiyo ni wazi kabisa kilichomtoa Guardiola kwenye dimba la Nou Camp si Barca kushindwa kunyakua taji msimu huu, ni kitu kingine kabisa kinachoanzia kwenye uongozi.
  Vita ya Rosell dhidi ya Laporta — mtu ambaye alimteua Guardiola — inaonekana kuhusika kwa namna fulani katika jambo hilo la Pep kuamua kutimka.
  Heshima ya Guardiola kwa Laporta haina kifani, lakini hiyo si sababu pekee iliyochangia kocha huyo kuamua kuondoka mwenyewe kabla ya Rosell kumwonyesha njia.
  Guardiola anafanya kazi saa 24 kwa wiki nzima na hivyo kukosa nafasi na muda wa kutosha wa kupumzika na familia yake.
  Licha ya kwamba hilo ni jambo la lazima, mazingira mengine katika Nou Camp yanaweka bayana kwamba hali si shwari kwa Guardiola kwamba hayupo kwenye mahusiano mazuri na baadhi ya wachezaji wake nyota, jambo ambalo si zuri.
  Lilikuwa ni suala la kawaida tu kwa Guardiola – ambaye alihitaji wachezaji wake kuwa na nidhamu ya kutosha na hivyo kuifikisha timu kwenye mafanikio inayostahili.
  Urafiki kwenye kikosi hicho ungemfanya Guardiola kuwa kwenye wakati mgumu wa kuwaonyesha baadhi ya wachezaji wake njia ya kutokea mwishoni mwa msimu huu.
  Baadhi ya wataalamu wa masuala ya soka wanaamini suala la kukichekecha kikosi hicho halikuwa la kupitwa na kwamba Barca inahitaji kuboresha kikosi chake mwishoni wa msimu huu kama kinahitaji kuwa na nguvu itakayowafanya kuendelea kupambana na kuonyesha kandanda la kishindani.
  Guardiola alitua kwenye kiti hicho akimbadili Frank Rijkaard mwaka 2008 na moja kwa moja akawaondoa wachezaji waliokuwa na ‘mapembe’ wake ule, Ronaldinho na Deco.
  Alifanya hivyo si kwamba nyota hao walishuka kiwango, hapana ni kwasababu hawakuwa wachezaji wake.
  Kwa wakati huu, Guardiola hakutaka kuuza wachezaji ambao alishirikiana nao muda wote na kufanikiwa kutwaa mataji yote yaliyopita mbele yao.
  Gerard Pique, mchezaji wa kwanza aliyesajiliwa na Guardiola, hakumchezesha kwenye mechi ya El Clasico iliyofanyika siku kadha zilizopita.
  Cesc Fabregas aliwekwa benchi kwenye mechi dhidi ya AC Milan kwenye dimba la San Siro na dhidi ya Bilbao na kwenye El Clasico.
  Kijamii, yote yalionekana kawaida – lakini kiwango cha Pique kipo kwenye mushkeli mkubwa na hilo linahitaji kuwapo ndani ya klabu hiyo kutambua kinachoweza kutokea siku za usoni.
  Hayo ni baadhi ya matukio ambayo, Guardiola angelazimika kumpiga bei Pique mwishoni mwa msimu, jambo lingekuwa gumu kwa kocha huyo.
  Nahodha wa zamani wa Arsenal, Cesc alipoteza nafasi mbili muhimu kabisa za mabao kwenye mchezo wao dhidi ya Stamford Bridge na alionyesha kiwango kibovu sana kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Chelsea — licha ya kwamba alipata penalti, ambapo Lionel Messi akashindwa kufunga.
  Mwingine ni Dani Alves, moja ya mabeki bora kabisa pembeni dunia. Huyu alitokea benchi kwenye mechi dhidi ya Chelsea.
  Kiwango cha Mbrazil huyo kimeshuka kwa asilimia kubwa na mazungumzo ya kutaka kuhamia Anzhi Makhachkala yamekuwa bayana kwa sasa.
  Fabregas ataendelea kubaki Nou Camp, hilo halina ubishi. Lakini, je, Pique na Alves watabaki? Pep hakutaka kuhusika kwenye kufanya uamuzi huo.
  Kingine, kuna suala la Rosell kutaka kumnunua Mbrazil, Neymar na Guardiola hataki. Kumsajili Neymar itakuwa ushindi mkubwa dhidi ya mahasimu wao Real Madrid.
  Lakini, Guardiola amekijenga kikosi chake kupitia Messi na hivyo hakutaka kuingiza mchezaji mwingine ambaye atasababisha mtikisiko kwenye vyumba vya kubadilishia nguo Nou Camp.
  Hayo ndio baadhi ya mambo yaliyomfanya Guardiola kuamua kumaliza nyakati zake katika kikosi hicho cha Barca.
  Kwa sasa ameshatangaza kuondoka na mengi yameanza kuhusishwa naye kuhusu hatima yake.
  Maneno kutoka Hispania yanabainisha kwamba Pep Guardiola anapenda kwenda kufanya kazi England.
  Si kufanya kazi England, si kufanya kazi Manchester United – bali England inayotajwa hapa ni timu ya taifa, Three Lions.
  Imebainika kwamba kocha huyo anaweza kushawishika kuchukua kibarua kingine kuliko maelezo yake ya awali ya kutaka mapumziko ya mwaka mmoja nje ya soka.
  Kuinoa timu ya taifa kumtafanya kuwa na muda wa kutosha wa kupumzika na familia yake kwasababu mechi ni chache na safari ni chache pia.
  Lakini, tatizo kubwa lililopo England ni kwamba Chama cha soka nchini humo (FA) kutaka kocha mzawa na juzi usiku walimbainisha Roy Hodgson kwamba ni chaguo lao namba moja.
  Lakini, kwa sasa kocha bora kabisa duniani yupo huru na hivyo FA wanatambua nafasi ipo wazi kwenye timu yao ya taifa, haitakuwa makosa kama wataweka pembeni suala la uzawa na kumchukua bosi huyo.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NINI HASWA KIMEMFANYA PEP GUARDIOLA AACHIE NGAZI BARCA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top