• HABARI MPYA

  Monday, April 30, 2012

  AZAM WALIVAA TOTO LA YANGA LENYE NGUVU ZA SIMBA LEO

  John Bocco Adebayor wa Azam kushoto, je leo ataingarisha Azam?
  KAMA kuna mechi ambayo Azam ina umuhimu mkubwa basi ya leo dhidi ya Toto Africans ina umuhimu wake katika mbio za kuelekea kwenye ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara. 

  Azam ina pointi 53 inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi nyuma ya vinara Simba wenye pointi 59, hivyo kama Azam itashinda leo itafikisha pointi 56 na itakuwa na mechi moja mkononi dhidi ya Kagera Sugar Jumamosi, hivyo ikishinda itafikisha pointi 59 na kuomba Simba ifungwe na Yanga Jumamosi ili zihesabiane uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa kuamua bingwa wa msimu huu. 

  Lakini kama Toto Africans ikiifunga ama kutoka sare na Azam leo itakuwa imeitangazia ubingwa Simba kabla ya ligi hiyo kumalizika, hivyo mchezo wake wa Jumamosi dhidi ya Yanga utakuwa wa kukamilisha ratiba. 

  Kutokana na mazingira hayo mchezo wa leo utakaofanyika Uwanja wa Azam Chamazi utakuwa wa ushindani mkubwa kutokana na timu zote mbili kuuchukulia umuhimu mkubwa kwa vile Toto Africans yenye pointi 26 inashika nafasi ya tano kutoka mkiani ikiwa pia haipo salama sana kwenye zile timu zilizopo kwenye hatari ya kushuka daraja. 

  Tayari Simba wametangaza azma yao ya kuiunga mkono Toto leo na jana Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga aliwatangazia mashabiki wa Simba Uwanja wa Taifa waende Chamazi wakashuhudie Toto anavyomfunga Azam.

  Habari zisizo za kuaminika zinasema Toto wamepewa sapoti kubwa ya maandalizi na Simba kwa ajili ya mchezo wa leo. 

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM WALIVAA TOTO LA YANGA LENYE NGUVU ZA SIMBA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top