• HABARI MPYA

    Friday, April 27, 2012

    MOGELLA JINA KUBWA LAKINI ALIIFUNGA YANGA BAO MOJA TU MAISHA YAKE YOTE


    Zamoyoni Mogella
    ZAMOYONI Mogella amewahi, hajawahi kuifunga Yanga?
    Mpachika mabao mashuhuri wa zamani nchini, Mogella aliyezaliwa miaka 58 iliyopita mjini Morogoro, amekuwa gumzo kubwa hata baada ya kustaafu kwake soka.
    Kumekuwa na ubishi kuhusu nyota huyo kwamba aliwahi au hajawahi kuifunga Yanga. Ukweli ni kwamba, Mogella aliifunga Yanga, tena lilikuwa bao ambalo lilielekea kuipa ushindi wa jumla wa mchezo huo Simba.
    Ilikuwa ni Julai 14, mwaka 1984 kwenye Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru mjini Dar es Salaam, wakati Golden Boy alipotangulia kuifungia Simba kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, sasa Ligi Kuu katika dakika ya 17.
    Hata hivyo, mchawi wa vichwa enzi hizo, Abeid Mziba aliisawazishia Yanga bao hilo katika dakika ya 39.
    Kabla ya kujiunga na Simba, Mogella alichezea timu za Jogoo, Reli, Tumbaku zote za Morogoro tangu mwaka 1974, hadi mwaka 1981, alipotua Mtaa wa Msimbazi.
    Alijiunga na Simba baada ya soka yake kuwavutia viongozi wa Simba alipokuwa akichezea timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20. Mogella aling'ara zaidi alipokwenda na timu hiyo kwenye michuano maalumu ya vijana iliyofanyika nchini Norway.
    Alitua Simba kwa dau la Sh 50,000 tu, ambayo tena alilipwa kwa awamu, kwanza 25,000 na nyingine akamaliziwa baadaye.
    Tangu anajiunga na Simba, Mogella pia alianza kuichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars. 
    Mwaka 1986, Mogella alikwenda kucheza soka ya kulipwa nchini Kenya katika klabu ya Volcano na baada ya miezi sita alikwenda Oman ambako alicheza hadi mwaka 1989.
    Alirejea Simba mwaka 1990 na aliichezea hadi mwaka 1992, alipohamia Yanga ambako alicheza kwa msimu mmoja tu.
    Ingawa wengi wanajua Athumani Juma Chama 'Jogoo' ndiye pekee aliyekuwa akimpa wakati mgumu Mogella uwanjani, lakini mwenyewe anawataja pia Yussuf Ismail Bana, Allan Shomari na Isihaka Hassan kwamba nao walikuwa wakimuumiza kichwa
    Hivi sasa Mogella ni baba wa watoto wanne, akiwemo Farshed, anayefuata nyayo za baba yake kwenye soka.
    Farshed, aliyezaliwa miaka 17 iliyopita, mbali na kucheza soka shuleni kwao, pia anachezea timu ya mtaani, Buibui nafasi ya ushambuliaji kama baba yake. Farshed ana pacha wake, Fuhal, aliyehitimu kidato cha Nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari Green Acres. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MOGELLA JINA KUBWA LAKINI ALIIFUNGA YANGA BAO MOJA TU MAISHA YAKE YOTE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top