• HABARI MPYA

    Wednesday, April 25, 2012

    KWA NINI IWE AZAM TU?


    Wachezaji wa Azam FC, timu ambayo inaongoza mechi zake za Ligi Kuu kuvurugika

    KWA mara ya tatu katika kipindi cha miezi miwili, juzi refa aliyechezesha mechi ya Azam FC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, alikuwa chanzo cha matatizo mchezoni.
    Mtibwa waligomea mechi na kuondoka uwanjani wakiwa wamefungana 1-1 na Azam FC, Uwanja wa Azam, Chamazi.
    Msimu uliopita Mtibwa Sugar walifungwa nyumbani na Azam mabao manne, hawakuleta tatizo, lakini juzi wakiwa wapo 1-1 wakaamua kugoma.
    Waligoma baada ya kuchoshwa na maamuzi mabovu ya refa, ikiwemo kuwapa penalti ambayo si halali wenyeji.
    Hii ni mara ya tatu ndani ya miezi miwili, marefa wanaochezesha mechi za Azam wanakuwa sababu ya kuvurugika kwa mchezo.
    Wiki mbili zilizopita tu, refa aliyechezesha mechi kati ya Azam FC na wenyeji Polisi Dodoma, Uwanja wa Jamhuri alipigwa na mashabiki baada ya mechi.
    Azam ilishinda 1-0, beo pekee la beki wake wa kati wa kimataifa wa Tanzania, Aggrey Morris Ambroce dakika ya 83 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Polisi Dodoma.
    Katika mchezo huo, Polisi Dodoma, ilipata pigo baada ya beki wake, Bakari Omari kutolewa nje kwa kadi nyekundu, dakika ya 57 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
    Refa  wa mchezo huo alipigwa na mashabiki kwa madai ya kuwapendelea Azam, baada ya mpambano kukamilika, lakini askari walifanikiwa kumuokoa asipokee kipondo zaidi.
    Awali, mwezi uliopita, refa aliyechezesha mechi kati ya Yanga na Azam, Israel Nkongo alipigwa na Stefano Mwasyika na angeweza kupigwa pia na mashabiki wa Yanga.
    Kwa nini apigwe? Kisa kutuhumiwa kuipendelea Azam. Mechi zinazochezwa kwenye Uwanja wao, timu nyingi zimekuwa zikilalamika Azam inabebwa.
    Kwa muda mrefu wapenzi wa soka Tanzania wamekuwa wakilalamikia desturi ya klabu kongwe nchini Simba na Yanga kutamba nyumbani, kudaiwa kushinda kwa kununua mechi.
    Hii inasababisha timu zetu zinakuwa dhaifu kwenye michuano mikubwa na ndiyo maana zinashindwa japo kucheza hatua ya makundi tu ya michuano ya Afrika.
    Watu wanataka timu ishinde kwa uwezo, ili idhihirishe ubora ambao utakwenda kuifanya ishiriki vyema michuano ya Afrika.
    Kwa sababu hiyo, ujio wa Azam FC timu inayomilikiwa na Milionea Said Salim Bakhresa ulipokewa kwa furaha na wadau wa soka nchini, wakijua amepatikana mkombozi wa kweli.
    Azam imewekeza fedha nyingi kuanzia kwenye usajili, ajira za makocha, Uwanja wake kule Chamazi- na kwa ujumla ni timu ambayo ukiangalia inapoelekea unajenga matumaini.
    Azam haina wanachama wa kuleta mizengwe ya kuvuruga timu, wanaweza kujivuruga wao kwa wao tu.
    Mchezaji wa Azam hachezi kwa presha ya kutukanwa na mashabiki akikosea kama mchezaji wa Yanga au Simba. Azam imesajili wachezaji nyota kuanzia ndani na nje ya nchi.
    Azam inaongoza kutumia fedha nyingi na kusajili wachezaji bora nchini. Hivyo timu hii inastahili kuwa bingwa wa nchi kulingana na jinsi ilivyowekeza.
    Lakini wasiwasi ni kwamba, mechi zao zinatiliwa shaka sasa nao kama wanatumia mbinu chafu ikiwemo kuhonga marefa ili kushinda.
    Kama kweli watakuwa wanafanya hivyo, ina maana watakuwa wanaiga Simba na Yanga, ambazo kimsingi zinanyooshewa kidole kwa kudumaza maendeleo ya soka ya nchi hii. 
    Kama Azam wanaiga Simba na Yanga kununua mechi, wanaweza wakafanikiwa kuwa mabingwa, lakini swali la kujiuliza soka ya Tanzania itakuwa kweli imepata mkombozi?
    Napata shaka sana juu ya mustakabali wa soka ya nchi hii, ikiwa Azam nayo inakuja kwa staili hii- dhahiri  bado tuna kazi ngumu na safari ndefu kufikia japo karibu na mafanikio.
    Kwa sababu mchezaji akishajua kwamba kuna unafuu katika mchezo kutokana na mabosi wao kuhonga, hawezi kujituma tena kwa sababu anajua ushindi upo tu.
    Mwaka 2007, baada ya Yanga kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Esperance ya Tunisia, aliyekuwa kipa wa timu hiyo, Ivo Mapunda aliwashauri viongozi wa klabu yake wakati huo, wawe wanafanya mipango na marefa kurahisisisha mechi.
    Tayari mchezaji kujenga dhana hiyo- inamaanisha amefikia mwisho wa uwezo wake, wakati suluhisho ni kufanyia kazi mapungufu ili wakati mwingine ufanye vizuri.
    Mwaka juzi, Simba ilifungwa 5-0 na Haras El Hodood nchini Misri katika mchezo wa Kombe la Shirikisho,  mwaka jana ilifungwa 3-0 na Wydad Cassablanca, mara zote ikitolewa katika michuano ya Afrika.
    Mwaka huu, imefungwa 3-1 ikitoka kushinda 2-0 nyumbani na ES Setif moja ya timu tishio tu Afrika na kuingia hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho.
    Hii nini maana yake? Simba imefanyia kazi mapungufu kutoka kufungwa 5-0, 3-0 na 3-1 sambamba na kusonga mbele.     
    Lakini desturi ya kutaka kurahisisisha kazi kwa kununua mechi- maana yake hatuwezi kufanyia kazi mapungufu.
    Kweli wapenzi wa soka Tanzania wanaitegemea Azam iijengee heshima nchi hii katika michuano ya Afrika, lakini kwa staili ambayo wanataka kwenda nayo. Hakuna hakika kama watafanikiwa.
    Yapo maneno tayari yanasemwa semwa kuhusu Azam na harakati zao za ubingwa na mbinu wanazodaiwa kutumia hadi watu wanaodaiwa kutumiwa kutoka kwenye mamlaka husika- japo kwa sasa tunayachukuliwa kama maneno ya mtaani tu, lakini ipo haja ya kuiangalia Azam kwa jicho la tatu.
    Haina maana Yanga kukosekana michuano ya Afrika mwakani, wakati ilipigana kwa uwezo wake na kuzidiwa na timu ambayo ushindi wake ulitokana na mbeleko za marefa.
    Namna hii hata mtu huwezi kustaajabu kwa nini John Bocco mabao yake anafunga Azam tu na timu ya taifa anabaki yeye na kipa mara kibao anashindwa. Akizomewa eti anasusa.
    Watu hawataki kujadili ukweli wa kiini cha tatizo, kwa sababu tayari kuna kosa lilitendeka- lakini hawajui kwamba hata kosa lina sababu.
    Jasiri yoyote hakubali kudhulumiwa haki yake bana- tusidanganyane na wala watu wasitake kujiona wao miungu watu katika dunia hii- misingi ya haki ni ile ile.
    Kila jina zuri lina jina mbadala la uasi- watu wakikupenda kwa ujasiri wako wa kutopenda kuonewa kiasi cha kuwa tayari kupambana na yeyote kutetea haki, watakuita jasiri, shujaa, shupavu.
    Lakini kwa sababu hizo hizo, wakiwa hawakupendi watakuita mkorofi- mgomvi, huelewani na watu- hiyo ndio dunia yetu ya leo- dunia tofauti na ile waliyoishi akina Mtemi Mirambo, Chifu Mkwawa na Adolph Hitler.
    Mtibwa walikuwa wastaarabu wakaondoka uwanjani- hawajui mbali na kupoteza pointi tatu, watatozwa faini na sijui kanuni zinasemaje zaidi, ili kuna hatari ya kufungiwa pia kucheza ligi.
    Wachezaji wa Yanga waliona bora kumtandika Nkongo- hawakujua mbele yake kuna kufungiwa kucheza na kuigharimu zaidi klabu yao.
    Lakini chanzo cha yote haya ni nini? Azam hao. Wanafanya nini, sijui na sina ushahidi kama wanahonga marefa na siwezi kusema wanahonga marefa, ila naweza kujiuliza kwa nini wawe wao tu? Mara moja bahati mbaya- lakini sasa mara ya tatu jamani, timu hiyo hiyo moja! Hapana bwana!
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA NINI IWE AZAM TU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top