• HABARI MPYA

    Tuesday, April 24, 2012

    BIN KLEB: ILIKUWA NIONDOKE NA MOSHA


    Bin Kleb kushoto, akimkabidhi Niyonzima jezi baada ya kumsainisha mwaka jana Kigali, rwanda

    MJUMBE wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema kwamba ilikuwa ajiuzulu siku nyingi, baada ya Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davis Mosha kujiuzulu, Machi mwaka jana.
    Akizungumza na bongostaz.blogspot.com, Bin Kleb alisema kwamba amekuwa akivumilia mambo mengi ya uongozi, alkini imefikia wakati anaamua kujiweka pembeni.
    “Ilikuwa niondoke muda mrefu tu tangu wakati ule Mosha alipojiuzulu, lakini nikavuta subira, ila kwa sasa nimefikia mwisho.
    Bin Kleb na Jumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Seif Ahmad ‘Magari’, ambaye ni swahiba wake kipenzi wamewasilisha barua za kujiuzulu wadhifa wao huo wa kuteuliwa.
    Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ameiambia bongostaz.blogspot.com mchana huu kwamba, ameambiwa juu ya Wajumbe hao wa Kamati ya Mashindano, kuwasilisha barua za kujiuzulu.
    Alipoulizwa sababu zilizoainishwa na watu hao kwenye barua zao, Nchunga alisema kwamba ni kutokuwana imani na uongozi.
    “Alipokuwa akizungumza na Radio One jana, alisema ni kwa sababu za kifamilia, lakini katika barua niliyosomewa na Katibu (wa Yanga, Celestine Mwesigwa), Seif amesema haridhishwi na mambo yanavyokwenda kwenye  uongozi,”alisemsa Nchunga akiinukuu barua ya Seif.
    “Anasema hapati taarifa za fedha kutoka kwa Katibu. Anasema fedha nyingi zinaingia Yanga, lakini yeye hajulishwi, wakati wao wanatumia fedha nyingi kugharamia klabu,”alisema Nchunga.
    Nchunga alisema yeye alikuwa safarini Afrika Kusini na amerejea jana, lakini hajaziona rasmi hizo barua bali amesomewa na Katibu Mkuu.
    Lakini alipoulizwa maoni yake juu ya madai ya Seif, kwanza Nchunga alisema; “Kwanza nataka niseme, huu haukuwa wakati mwafaka kuleta haya mambo, tuna wiki mbili kabla ya kucheza na Simba. Hizi ni dalili mbaya,”alisema.
    Kuhusu madai ya Seif kutojulishwa taarifa za fedha, Nchunga alisema kwamba taarifa za fedha zinatolewa katika vikao vya Kamati ya Utendaji.
    “Na sisi tunakutana sana, na kama mtu anataka kuhoji jambo, hakatazwi, sasa sielewei hii inatoka wapi,”alisema.
    Lakini Nchunga alisema inawezekana matokeo mabaya msimu huu yamechafua hali ya hewa ndani ya Yanga kiasi kwamba viongozi hao wameshindwa kuimudu.
    “Kuna mengi katika wakati huu timu ikiwa vibaya, kuna kuzongwa na wanachama na nini, ni mambo ambayo viongozi wanatakiwa kuvumilia na tujipange upya kwa ajili ya mashindano yajayo, lakini si kujiuzulu,”alisema Nchunga.
    Pamoja na hayo, Nchunga alisema kwamba anawatafuta kwanza viongozi hao azungumze nao na kujaribu kuwashawishi warudi katika uongozi.
    “Nina wajibu wa kufanya jitihada za haraka ili kunusuru mmomonyoko huu usitokee, huu ni wakati ambao wana Yanga tunapaswa kushikamana sana ili kuinusuru klabu yetu, hapa ninatoka kuanza kuhangaikia hilo,”alisema Nchunga.
    Yanga ipo katika wakati mgumu hivi sasa, baada ya kukosa nafasi ya kucheza ya michuano ya Afrika mwakani, ikizidiwa kete na Azam FC.
    Yanga ilipoteza nafasi hiyo, baada ya kupoteza pointi tisa mfulilizo katika mechi dhidi ya Coastal Union, Toto African na Kagera Sugar.
    Pamoja na kuifunga Coastal bao 1-0, lakini Yanga ilipokonywa pointi kwa kosa la kumtumia beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akiwa anatumikia adhabu kabla ya kwenda kufungwa 3-2 na Toto na 1-0 na Kagera.
    Seif na Bin Kleb ni watu muhimu mno ndani ya Yanga kwa sasa, ambao wazi kama wataachia ngazi klabu itayumba na kuna hatari ya kupoteza malengo ya msimu ujao.
    Achilia mbali ujanja wao wa mjini unaowawezesha kupambana na fitina za wapinzani wao katika Ligi Kuu, lakini wamekuwa wakihudumia timu kuanzia usajili na uendeshaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BIN KLEB: ILIKUWA NIONDOKE NA MOSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top