• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 27, 2012

  TANGU 1977 REKODI YA KIBADENI HAIJAVUNJWA SIMBA NA YANGA

  Kibadeni wa tatu kutoka kushoto
  KUCHEZA Simba au Yanga ni fahari kwa mchezaji wa Tanzania. Lakini ni fahari zaidi iwapo atakuwa mchezaji ambaye atashiriki mechi baina ya timu hizo.
  Inakuwa fahari zaidi iwapo mchezaji atafunga bao au mabao katika mechi ya watani wa jadi, kwani huwafanya maelfu ya mashabiki wa timu yake walitaje jina lake na kushangilia kwa raha zao. Wengine, hupewa zawadi kutokana na kufunga kwenye mechi hizo za watani.
  Wapo waliolewa sifa na kupotea kwenye ramani ya soka haraka, kwa sababu tu ya kuvimba kichwa baada ya kufunga mabao mfululizo kwenye mechi za watani.
  Said Sued 'Scud', alifunga bao pekee la ushindi kwenye mechi ya watani wa jadi, akiwa anaichezea Yanga alitikisa nyavu za Simba dakika ya saba katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, sasa Ligi Kuu Mei 18, mwaka 1991.
  Huo ukiwa msimu wake wa kwanza kwenye klabu hiyo, hakika ilikuwa furaha kubwa kwake, kwani tangu hapo aliaminika na kuwa mchezaji wa kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.
  Chipukizi huyo wa wakati huo, alipata ngekewa ya kuifunga tena Simba katika mchezo uliofuata wa marudiano wa ligi baina ya watani wa jadi, likiwa pia bao pekee la ushindi Agosti 31, mwaka huo huo 1991, jambo ambalo lilimfanya awe maarufu zaidi.
  Lakini katika mastaajabu ya wengi, Scud hakurejea kwenye kikosi cha Yanga cha mwaka 2002 na huo ukawa mwisho wa umaarufu wake kwenye soka ya Tanzania.
  Kama wapo wanaodhani Scud alifanya kubwa sana katika historia ya watani wa jadi, watakuwa wapo mbali kabisa na ukweli, kwani Abdallah Kibadeni (pichani kulia juu), maarufu kama Chifu Mputa ama King, au Ndululu kama walivyokuwa wakimuita Wakenya, anaweza kusimama na kusema ana kubwa la kujivunia katika historia ya mechi baina ya Simba na Yanga ambalo hadi kitabu hiki kinaingia sokoni lilikuwa halijavunjwa.
  Abdallah Kibadeni ndiye mchezaji pekee hadi sasa aliyeweza kufunga mabao matatu peke yake katika mchezo mmoja kwenye mechi za watani wa jadi katika Ligi.
  Hiyo ilikuwa ni Julai 19, mwaka 1977 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, sasa Uwanja wa Uhuru, wakati Yanga ilipotandikwa 6-0 na Simba.
  Siku hiyo, Kibadeni alitikisa nyavu za Yanga katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mabao mengine ya Wekundu wa Msimbazi, yalitiwa kimiani na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika ya 60 na 73 na jingine Selemani Sanga wa Yanga alijifunga mwenyewe dakika ya 20 katika harakati za kuokoa krosi ya Ezekiel Greyson 'Jujuman'.
  Hivyo siku hiyo mbali na Simba kushangilia kulipa kisasi cha kulala 5-0 kwa Yanga, Juni Mosi mwaka 1968, Kibadeni alikuwa ana sherehe binafsi za kutumbukiza tatu peke yake kwenye mechi baina ya watani hao, jambo ambalo liliwashinda wengi kabla yake kati ya waliowahi kuvaa jezi za Simba au Yanga.
  Hakuna cha Sunday Manara 'Computer' wala Maulid Dilunga 'Mexico' aliyewahi kufanya hivyo zaidi ya King Kibadeni pekee.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TANGU 1977 REKODI YA KIBADENI HAIJAVUNJWA SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top