• HABARI MPYA

    Monday, April 30, 2012

    WAZEE YANGA WATEPETA, NCHUNGA AENDELEA KULA BATA JANGWANI


    Kikosi cha Yanga

    YANGA imeanza mazoezi leo baada ya mapumziko ya siku kadhaa, chini ya uongozi halali uliochaguliwa kikatiba, chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga.
    Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu ameiambia BIN ZUBEIRY blog kwamba wachezaji wote wa timu hiyo walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Tiper, Kigamboni, Dar es Salaam leo asubuhi.
    Sendeu alisema kwamba program ya mazoezi itaendelea kesho asubuhi na baada ya mazoezi hayo, timu itaingia kambini moja kwa moja.
    Alipoulizwa kuhusu mpango wa Baraza la Wazee kuchukua timu, Sendeu alisema; “Mimi sijui kuhusu wazee wamefikia wapi, nachojua timu bado ipo chini ya uongozi halali, uliochaguliwa kikatiba chini ya Mwenyekiti wake nchinga,”alisema.
    Jana, Nchunga aliwaambia Baraza la Wazee la klabu hiyo, waliotaka kuichukua timu kufuatia mgogoro unaoendelea klabuni, akisema wamuonyeshe vielelezo vya vyanzo vyao vya mapato awape timu.
    Lakini Nchunga amekataa ombi au taarifa ya kujiuzulu kwa Mjumbe wa Kamati ya Usajili na Kamati ya Mashindano, Abdallah Ahmed Bin Kleb, wakati huo huo akimkubalia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Seif Ahmad Magari kuachia ngazi.
    Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari asubuhi ya jana, makao makuu ya klabu makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Wakili Nchunga alisema kwamba Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha juzi ilikubali kujiuzulu kwa Seif, lakini imekataa kwa Bin Kleb.
    Kuhusu Wazee kuchukua timu, Nchunga alisema kweli alifanya nao kikao na akawaambia atakuwa tayari kuwaachia timu waihudumie kwa mujibu wa Katiba, lakini kwanza lazima watoe vielelezo juu ya vyanzo vyao fedha ili ajue uhalali wake, wasije wakaiingiza klabu kwenye matatizo.
    Alisema anahofia wasije wakawa wanapata fedha kutoka kwa watu wenye kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya- wakaiingiza Yanga kwenye matatizo.
    Nchunga alisema iwapo watamuhakikishia vyanzo halali vya mapato, kwa mujibu wa Katiba atawaachia jukumu la kuihudumia timu na si kuhodhi madaraka ya uongozi.
    Kwa kuwa Wazee walitaka kuanzia kazi kwenye mechi dhidi ya Simba Mei 5, mwaka huu, maana yake wakipewa timu, wao wataihudumia, lakini mapato ya mechi watachukua akina Nchunga.
    Baada ya kuifunga JKT Oljoro 4-1 wiki hii, wachezaji wa Yanga walipewa mapumziko na juzi walikusanyika tayari kuanza mazoezi, ingawa walikwama kwa sababu ya mvua.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAZEE YANGA WATEPETA, NCHUNGA AENDELEA KULA BATA JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top