• HABARI MPYA

    Monday, April 30, 2012

    NCHUNGA AIPELEKA YANGA KAMBINI KWA JAKAYA


    Kikosi cha Yanga

    YANGA SC inaingia kambini Bagamoyo mkoani Pwani, anakotokea rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kesho mapema tu, kujiandaa na mpambano wa funga dimba Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC Mei 5, mwaka huu.
    Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ameiambia BIN ZUBEIRY blog (bongostaz.blospot.com) muda mchache uliopita kwamba yeye mwenyewe ataongoza timu kwenda kambini.
    “Nitakwenda na timu Bagamoyo kesho kwa ajili ya maandalizi ya kuua mnyama Mei 5, tumekosa ubingwa, lakini tunataka heshima, lazima tuue mnyama,”alisema Nchunga.
    Leo Yanga ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Tiper, Kigamboni, Dar es Salaam leo asubuhi.
    Kitendo cha Nchunga kupeleka timu kambini Bagaamoyo, kinaashiria Baraza la Wazee la klabu hiyo limekwama kuiteka timu kama lilivyodhamiria.
    Mapema jana, Nchunga aliwaambia Baraza la Wazee la klabu hiyo, waliotaka kuichukua timu kufuatia mgogoro unaoendelea klabuni, akisema wamuonyeshe vielelezo vya vyanzo vyao vya mapato awape timu.
    Lakini Nchunga amekataa ombi au taarifa ya kujiuzulu kwa Mjumbe wa Kamati ya Usajili na Kamati ya Mashindano, Abdallah Ahmed Bin Kleb, wakati huo huo akimkubalia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Seif Ahmad Magari kuachia ngazi.
    Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari asubuhi ya jana, makao makuu ya klabu makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Wakili Nchunga alisema kwamba Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha juzi ilikubali kujiuzulu kwa Seif, lakini imekataa kwa Bin Kleb.
    Kuhusu Wazee kuchukua timu, Nchunga alisema kweli alifanya nao kikao na akawaambia atakuwa tayari kuwaachia timu waihudumie kwa mujibu wa Katiba, lakini kwanza lazima watoe vielelezo juu ya vyanzo vyao fedha ili ajue uhalali wake, wasije wakaiingiza klabu kwenye matatizo.
    Alisema anahofia wasije wakawa wanapata fedha kutoka kwa watu wenye kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya- wakaiingiza Yanga kwenye matatizo.
    Nchunga alisema iwapo watamuhakikishia vyanzo halali vya mapato, kwa mujibu wa Katiba atawaachia jukumu la kuihudumia timu na si kuhodhi madaraka ya uongozi.
    Kwa kuwa Wazee walitaka kuanzia kazi kwenye mechi dhidi ya Simba Mei 5, mwaka huu, maana yake wakipewa timu, wao wataihudumia, lakini mapato ya mechi watachukua akina Nchunga.
    Baada ya kuifunga JKT Oljoro 4-1 wiki hii, wachezaji wa Yanga walipewa mapumziko na juzi walikusanyika tayari kuanza mazoezi, ingawa walikwama kwa sababu ya mvua.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NCHUNGA AIPELEKA YANGA KAMBINI KWA JAKAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top