• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 29, 2012

  SIMBA MGUU MOJA MBELE AFRIKA


  Kikosi cha Simba kilichofanya mauaji leo taifa, kutoka kulia waliosimama Emanuel Okwi, Juma Kaseja, Haruna Moshi, Uhuru Suleiman, Patrick Mafisango na Felix Sunzu. Walioinama kutoka kulia Kelvin Yondan, Shomari Kapombe, Amir Maftah, Nassor Masoud na Mwinyi Kazimoto. 
  SIMBA SC imejiwekea mazingira mazuri ya kuingia kwenye hatua ya Nane Bora ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, baada ya kuifunga Al Ahly Shandy mabao 3-0 jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Simba sasa inahitaji sare yoyote kwenye mchezo wa marudiano, au kufungwa si chini ya mabao 2-0 ili kuingia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo.
  Timu nane zitakazotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa zitaungana na timu nane zitakazofozu katika hatua hii ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, kuchuana kuwania nafasi nane za kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
  Simba leo ingeweza kuondoka na ushindi mnono zaidi wa mabao 5-0, kama si kupoteza penalti kipindi cha kwanza na nafasi moja ya wazi mno kipindi cha pili.
  Kipindi cha kwanza cha mchezo huo, kilikuwa kigumu kwa Simba, lakini baada ya kupata mawaidha ya kocha wao, Profesa Milovan Cirkovic, Simba waliingia na mvua ya mabao kipindi cha pili na kuufanya Uwanja wenye uwezo wa kumeza mashabiki 60,000 uchangamke.
  Bao la kwanza la Simba lilifungwa na Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’, dakika ya 66 baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Felix Mumba Sunzu Jr.
  Sunzu alipokea pasi ndefu ya Uhuru Suleiman Mwambungu, ambaye aliuwahi mpira uliookolewa baada ya Simba kushambuliwa.
  Sunzu alifanya kazi nzuri ya kumtoka beki wa Shandy, Fareed Mohamed kabla ya kumpa pasi mfungaji.
  Bao la pili la Simba lilifungwa na Patrick Mutesa Mafisango, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Emmanuel Arnold Okwi kuwatoka mabeki wa Shandy.
  Bao la tatu la Simba lilipatikana dakika ya 86, mfungaji Emanuel Okwi kufuatia gonga safi ya wachezaji wa Simba kwenye eneo la hatari la Shandy.
  Boban alikaribia kufunga tena kabla ya hapo, baada ya kupewa pasi nzuri akiwa amebaki yeye na kipa, lakini akapiga juu ya lango.
  Dakika ya 75, Juma Kaseja ‘Tz One’ alidaka krosi ya Razak Yakubu kichwani kwa Nadir Eltaveeb, hilo likiwa shambulizi pekee la hatari la Shandy kipindi cha pili.
  Hadi mapumziko, hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake, Al Ahly Shandy wakitawala zaidi mchezo na kupoteza nafasi nyingi za wazi.
  Katika kipindi hicho, Simba walipoteza penalti, baada ya mkwaju wa kiungo Patrick Mutesa Mafisango kuokolewa na kipa wa Shandy, Abdulrahman Ali dakika ya 38.
  Penalti hiyo ilifuatia mshambuliaji Emmanuel Okwi kuangushwa kwenye eneo la hatari na kipa Ali, baada ya kuwatoka mabeki wa timu hiyo ya Sudan.
  Kipindi cha kwanza Ahly ndio waliotawala mchezo kutokana na kuwazidi Simba katika eneo la kiungo.
  Walikuwa wakicheza soka ya utulivu na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, ingawa bahati haikuwa yao.
  Dakika ya sita Shandy walishambulia vizuri langoni mwa Simba, lakini shuti dhaifu la kiungo wake wa kushoto Bassiro Ubamba lilidakwa na kipa wa Simba, Juma Kaseja.
  Dakika ya tisa, beki Kelvin Yondan alitolewa nje na refa akarekebishe namba ya jezi yake ambayo ilikuwa imebanduka na kutoonekana vizuri.
  Benchi la ufundi la Simba lilitumia dakika tatu kutengeneza namba hiyo ya jezi, muda wote huo Simba ikicheza pungufu.
  Dakika ya 19, Nadir Eltaveb alipiga shuti zuri nje ya 18, lakini Kaseja alipangua ikawa kona ambayo haikuzaa matunda.
  Dakika ya 22, Ubamba alifumua shuti kali kutoka wingi ya kushoto likatoka nje sentimita chache.
  Dakika ya 28, Simba ilizinduka na wachezaji wake Haruna Moshi ‘Boban’, Mwinyi Kazimoto na Shomary Kapombe waligongeana vizuri, kabla ya kumpa Mafisango aliyetoa pasi ya mwisho kwa kubetua juu mpira, lakini beki Fareed Mohamed akabinuka tik-tak na kuondosha hatarini.
  Dakika ya 41, krosi nzuri ya Amir Maftah ilisababisha piga nikupige langoni mwa Shandy- mpira ulikaribia kuvuka mstari, lakini wakati wachezaji wa Al Ahly wakizuia, Okwi, Uhuru Suleiman, Felix Sunzu na Boban walikuwa wakijaribu kuusukuma nyavuni, hadi kipa akadaka.
  Hata hivyo, kipa alidaka na kuumia- ilimchukua dakika mbili akitibiwa kabla ya kuinuka na kuendelea na mchezo.
  Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango, Uhuru Suleiman/Salum Machaku dk86, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi na Emmanuel Okwi.
  Al Ahly Shandy: Abdulrahma Ali, Elnour Altigani, Isaac Seun Malik, Saddam Abu Talib, Fareed Mohamed/Orwah Ibrahim dk 83, Zakaria Nasu, Razak Yakubu, Faris Abdallah, Hamopuda Bashir/Mogabid Farouq dk63, Nadir Eltaveb na Bashiro Ubamba.  

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  1 maoni:

  Bila jina alisema ... 29 Aprili 2012 18:45

  Shukrani mkuu kwa maelezo yako ya kina kabisa juu ya mpambano huo wa Simba.Lakini pia niwapongeze sana Simba kwa kuwapa raha watanzania, Mabao matatu ni ushindi mzuri hasa ukizingatia hawakuruhusu bao lolote naamini watajipanga vema kwa ajili ya mpambano wa marudiano
  Hongereni sana Simba.

  Item Reviewed: SIMBA MGUU MOJA MBELE AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top