• HABARI MPYA

  Jumatatu, Aprili 30, 2012

  CHELSEA INAVYOZIDI KUMUACHA 'UCHI' AVB


  Drogba ambaye chini ya AVB alionekana kafilisika kisoka

  ANDRE Villas-Boas ni lazima atakuwa ameketi huko aliko na kukuna kichwa chake kutokana na kile kinachoendelea kutokea Chelsea kwa sasa.
  Ni lazima atakuwa anashangwa na kile kinachoendelea kwenye klabu hiyo yenye maskani yake Stamford Bridge.
  Mreno huyo, AVB alitua Chelsea na kuanzisha vitu vipya kabisa kwenye kikosi hicho vya ndani na nje ya uwanja na kufanya filosofi iliyoonekana kuwa mtihani mgumu kueleweka na nyota wake.
  Aliwaweka kando wachezaji wazee, akawaingiza vijana na kutaka kucheza kwa nidhamu kubwa na soka la kisasa – huku akilenga kwenye mambo yajayo. Unafahamu nini kilimtokea?
  Chelsea ikawa kwenye wakati mgumu na timu ilishindwa kupata matokeo mazuri na hivyo kujikuta akionyeshwa mlango wa kutokea na bilionea mwenye timu yake, Roman Abramovich.
  Kuondoka kwake kumefungua njia kwa aliyekuwa msaidizi wake, Roberto Di Matteo kushika usukani. Muitaliano huyo anatambua namna ya kwenda na kikosi kama hicho cha Chelsea kilichoegemea zaidi kwa wachezaji wenye umri mkubwa.
  Di Matteo akatoa uhuru kwa wachezaji wake na kuacha kuwabana kwa mambo ya nje ya uwanja. Jambo hilo limeifanya timu hiyo kurudi kwenye makali yake na kuwa Chelsea tishio.
  Matokeo ya hilo. Chelsea sasa imekuwa ni moja ya timu hatari zaidi England na kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
  Kama timu hiyo ingeendelea kubaki chini ya AVB ni wazi hali ingekuwa mbaya zaidi kutokana na filosofi za Mreno huyo kutaka kuwaendeesha wachezaji wenye umri mkubwa kama Frank Lampard kama vile wangali watoto.
  Huwezi kumfundisha mambo ya kufanya Lampard anapokuwa kwenye shughuli zake za nje ya uwanja au kumbana kama utakavyofanya kwa kinda kama Daniel Sturridge, ambaye utahitaji awe na nidhamu ili kulinda kipaji chake kichanga.
  Tangu AVB alipoondoka na ‘vibabu’ vya Chelsea vimepata uhuru wao – vimeweza kuwa tishio na sasa zimetinga fainali ya Ligi ya Mabingwa barani na Kombe la FA.
  AVB aliwabana wachezaji hao – kitu ambacho awali alipata nguvu kubwa kutoka kwa bosi wake, Abramovich – kabla ya mambo kumgeukia na kuonyeshwa njia ya kutokea.
  RDM amechukua mikoba, amekikusanya kikosi hicho na kukirudisha pamoja kama kundi na hivyo kurejea kwenye kasi yao ya ushindi na ukichanganya na bahati ya Muitaliano huyo, basi mafanikio hayo yanamfanya aonekane ‘genius’.
  Ni hadithi inayofurahisha. Wakati AVB alipokwenda na kikosi chake cha Chelsea kumenyana na QPR Loftus Road – Oktoba mwaka jana, Jose Bosingwa na Didier Drogba walitolewa kwa kadi nyekundu, kadi saba za njano na Blues ilipokea mkong’oto wa 1-0.
  Kilikuwa ni kipindi ambacho hali ilikuwa mbaya zaidi ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo kwenye klabu hilo. Kipindi ambacho Fernando Torres alishindwa kutikisa nyavu na hivyo kuonekana kama hawezi kuvaa buti za Drogba katika kuisaidia timu hiyo.
  Na sasa miezi sita baadaye, unajua nini kimetokea? Maajabu mawili ndani ya wiki moja. Kwanza tukio lile la Nou Camp na sasa hili ambalo pengine ni kubwa zaidi, la kumfanya Torres kurejea kwenye kasi yake ya kufumua nyavu.
  Mhispania huyo alifunga ‘hat-trick’ yake ya kwanza tangu alipojiunga na timu hiyo na hivyo kuongeza kwa mara mbili mabao yake kwenye ligi.
  Na hapo Chelsea ikapata ushindi wake mkubwa kabisa kwa msimu huu, wakati walipoikung’uta QPR 6-1.
  Frank Lampard alicheza kwa kiwango kikubwa, Ashley Cole alicheza kama beki bora kabisa barani Ulaya na Bosingwa, ambaye alishindwa kuingia kwenye kikosi hicho – anacheza kama beki wa kizamani wa kati.
  Hiyo ni wazi kabisa kwamba baadhi ya wachezaji wakongwe na wenye uzoefu katika kikosi hicho hawakuwa tayari kucheza dhidi ya AVB.
  Wakati Chelsea inafunga bao lake la nne juzi, mvua ilinyesha na muda mfupi baadaye jua lilitoka jambo lililodhihirisha wazi kwamba hata Mungu yupo upande wa Di Matteo.
  Kutokana na yote hayo, kwanini Muitaliano huyo asitajwe kuwa kocha wa kudumu kwenye kikosi hicho?
  Kikosi hicho kwa sasa kipo kwenye fainali mbili. Je, nini hatima ya RDM kama ataweza kunyakua mataji yote mawili?
  Kwa matokeo yoyote yatakayotokea, Chelsea kwa sasa inafurahia nyakati nzuri kabisa zilizowahi kutokea kwenye kikosi chao ni wazi mafanikio haya ni kama yanamwacha mtupu AVB – ambaye alishindwa kuhamishia makali yake ya FC Porto kwenye klabu hiyo ya ‘darajani’.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHELSEA INAVYOZIDI KUMUACHA 'UCHI' AVB Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top