• HABARI MPYA

  Thursday, April 26, 2012

  DK TAMBA ALETA BUSARA KUINUSURU YANGA


  MJUMBE wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dk Maneno Tamba (pichani kushoto) amewaomba wapenzi na wanachama wa Yanga kushikamana katika wakati huu mgumu, wamalize Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara salama.
  Akizungumza na bongostaz.blogspot.com, Dk Tamba alielezea kusikitishwa kwake na kujiuzulu kwa Wajumbe wawili wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo, Seif Ahmad ‘Magari’ na Abdallah Ahmed Bin Kleb mwanzoni mwa wiki.
  Tamba alisema viongozi hao wanaondoka katika uongozi katika kipindi kigumu ambacho, timu imekosa nafasi ya kucheza michuano ya Afrika mwakani na inakabiliwa na mechi ngumu ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya watani wa jadi, Simba SC.
  “Nawaomba wanachama, wapenzi, wachezaji na viongozi, kushikamana na kuwa kitu kimoja haswa katika wakati huu wa kujiandaa na kucheza mechi ya mwisho na Simba.
  Na viongozi waliojiuzulu, au kutangaza kujitoa, nao huu si wakati mwafaka kufanya hivyo, na kama wapo wengine wanaotaka kufanya hivyo, nawaomba wasifanye kwa kipindi hiki,”alisema Dk Tamba.
  Tamba aliongeza; “Wao wana dhamana kubwa waliyopewa na wanachama wa Yanga, wakiwa wanataka kutoka, basi wasubiri tumalize ligi ndio watoke, mbele ya wanachama wa Yanga, mkutanoni, waseme yote mabaya na maovu,”aliasa Dk Tamba.
  Seif na Bin Kleb wamejiuzulu kwa sababu za kutoridhishwa na uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga.
  Wameelezea matatizo mengi katika kujiuzulu kwao, kubwa ni kutokuwa na imani na Mwenyekiti wao. Tayari Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Davis Mosha alijiuzulu Machi mwaka jana kwa sababu ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti wake huyo.
  Yanga imekosa nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye michuano ya Afrika mwakani, baada ya kuzidiwa kete na Azam FC.
  Walikuwa wana mwendo mzuri na mwelekeo wa ubingwa kabla ya kupoteza pointi tisa mfululizo, dhidi ya Coastal Union ya Tanga, Toto African ya Mwanza na Kagera Sugar ya Bukoba.
  Licha ya kuifunga Coastal 1-0 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga- Yanga ilipokonywa pointi tatu kwa kosa la kumtumia beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akiwa hajamaliza kutumikia adhabu yake ya kadi nyekundu kabla ya kwenda kufungwa na Toto mabao 3-2 na Kagera 1-0.
  Lakini baada ya hapo, Yanga imeshinda mechi zake mbili mfululizo kabla ya kumenyana na Simba, 3-1 dhidi ya Polisi Dodoma na 4-1 dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: DK TAMBA ALETA BUSARA KUINUSURU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top