• HABARI MPYA

    Sunday, December 09, 2018

    YANGA SC YATOKEA NYUMA TENA NA KUSHINDA 2-1 DHIDI YA BIASHARA UNITED YA MARA NA KUREJEA KILELENI LIGI KUU

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Biashara United ya Musoma mkoani Mara usiku wa leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 41 baada ya kucheza mechi 15, sawa na Azam FC wenye pointi 39 ambao wanarejea nafasi ya pili, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 27 za mechi 12 wanaendelea kushika nafasi ya tatu.
    Haukuwa ushindi mwepesi kwa Yanga SC inayofundishwa na kocha Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwani kwa mara ya pili mfululizo ililazimika kutokea nyuma baada ya kutanguliwa na wapinzani.
    Heritier Makambo (kushoto) akiwa mawindoni kwenye mchezo wa leo kabla ya kuifungia Yanga bao la ushindi 
    Mfungaji wa bao la kwanza la Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' akiwa juu kupiga mpira kichwa 
    Heritier Makambo akiwa ameruka juu dhidi ya kipa wa Biashara United Nourdine Balora
    Kikosi cha Yanga SC kilichoanza kwenye mchezo wa leo dhidi ya Biashara United  
    Kikosi cha Biashara United kilichoanza leo dhidi ya Yanga SC Uwanja wa Taifa

    Kama ilivyokuwa ikishinda 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons mjini Mbeya kwenye mechi iliyopita – na leo Yanga walitanguliwa kwa bao la Abdulmajjid Mangalo dakika ya 38 aliyawazidi mbio mabeki wa timu hiyo baada ya kutanguliziwa mpira mrefu, Biashara wakitoka kuzuia shambulizi la wenyeji.    
    Baada ya bao hilo, Biashara wakaendelea kucheza kwa kujilinda vizuri na kuzuia mashambulizi mengi ya Yanga SC kiasi cha mashabiki wa wenyeji kuanza kukata tamaa.
    Lakini kwa mara nyingine, Zahera akaonyesha weledi wake kwa mabadiliko yaliyokwenda kuiongezea kasi timu hadi kutokea nyuma tena na kushinda.
    Zahera ambaye pia ni Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya DRC, aliwatoa viungo Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mzimbabwe, Thabani Kamusoko na Raphael Daudi na kuwaingiza Mkongo mwenzake, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe.
    Na ni Tambwe aliyempasia beki Abdallah Hajji Shaibu ‘Ninja’ kuifungia Yanga SC bao la kusawazisha dakika ya 70, kama Mkongo Heritier Makambo kufunga bao la pili dakika ya 80.
    Makambo alifunga bao ambalo lingekuwa la tatu kama si refa kukataa akidai alimchezea rafu mchezaji wa Biashara kabla ya kufunga. 
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Paul Godfrey, Mwinyi Hajji Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum/Pius Buswita dk67, Thabani Kamusoko/Amissi Tambwe dk56, Heritier Makambo, Raphael Daudi/Papy Kabamba Tshishimbi dk41 na Jaffar Mohammed. 
    Biashara United; Nourdine Balora, Godfrey Mapunda/Kauswa Bernard Manumbu, Juma Mpakala, Abdulmajjid Mangalo, Sospeter Kasori, George Makang’a/Mpapi Nassib, Lameck Chamkaga, Frank Sekule/Taro Donald, Lenny Kissu, Wilfred Kourouma na Lambele Jerome. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YATOKEA NYUMA TENA NA KUSHINDA 2-1 DHIDI YA BIASHARA UNITED YA MARA NA KUREJEA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top