• HABARI MPYA

  Monday, January 05, 2015

  MESSI AIPELEKA SIMBA SC ROBO FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  SIMBA SC imefuzu Robo Fainali za Kombe la Mapinduzi kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi JKU katika mchezo wa Kundi C, uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Matokeo hayo yanaifanya Simba SC imalize kileleni mwa Kundi C kwa pointi zake sita baada ya mechi tatu, mbele ya Mtibwa Sugar iliyomaliza na pointi tano.
  Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika Simba SC wakiwa tayari wamepata bao hilo, lililofungwa na Ramadhani Singano ‘Messi’ dakika ya 12 kwa shuti kali akiwa ndani ya boksi baada ya kupewa pasi nzuri na Said Ndemla.
  Sifa zimuendee mshambuliaji Mganda, Dan Sserunkuma ambaye baada ya kupewa pasi na kiungo Jonas Mkude, aliwahadaa wachezaji wa JKU kabla ya kumpasia Ndemla aliyempa mfungaji.
  Mshambuliaji wa Simba SC, Elias Maguri akimiliki mpira mbele ya beki wa JKU Uwanja wa Amaan usiku huu
  Wachezaji wa Simba SC wakimpongeza mwenzao Ramadhani Singano 'Messi' (katikati) baada ya kufunga bao pekee

  Timu zote zilishambuliana kwa zamu kipindi cha kwanza na kosa kosa zilikuwa za pande zote mbili.  
  Kipindi cha pili mchezo ulizidi kunoga, Simba SC inayofundishwa na Mserbia Goran Kopunovic ikisaka mabao zaidi na JKU wakitafuta bao la kusawazisha.
  Hata hivyo, Simba SC walifanikiwa kuulinda ushindi wao na kusonga mbele, ambapo sasa watasubiri matokeo ya mwisho kesho kujua mpinzani wao katika Robo Fainali.
  Mechi za kesho, ni KCCA na KMKM, Azam FC na Mtende na Yanga na Shaba Uwanja wa Amaan, wakati Uwanja wa Mao dze Tung, Polisi itamenyana na Taifa Jang’ombe.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murushid, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’/Twaha Ibrahim, Said Ndemla, Elias Maguri/Abdi Banda dk90, Dan Sserunkuma/Ibrahim Hajibu dk78 na Awadh Juma/Shaaban Kisiga dk82.
  JKU; Mohammed Abraham, Ponsiana Malik, Suleiman Omar, Khamis Abdallah, Khamis Said/Nassor Juma dk86, Issa Haidari, Isihaka Othman, Amour Omar, Hilal Rehani/Mbarouk Fakhi dk61, Mohammed Abdallah/Mbarouk Chande dk62 na Ismail Khamis.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MESSI AIPELEKA SIMBA SC ROBO FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top