• HABARI MPYA

    Friday, June 06, 2014

    FEDHA ZA KAPOMBE ZAZUA BALAA MSIMBAZI, HANS POPPE ASEMA AZAM HAWAHUSIKI, MALIPO YAFANYWE NA AS CANNES

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameonya kiongozi yeyote wa Simba SC asipokee fedha za mauzo ya Shomary Kapombe kutoka Azam FC, bali malipo yafanywe klabu ya AS Cannes ya Ufaransa.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Poppe amesema kwamba Simba SC iliingia Mkataba na AS Cannes juu ya Kapombe na makubaliano yalikuwa akiuzwa wapewe asilimia 40.
    Poppe amesema amefanya uchunguzi amegundua Azam FC imemnunua Kapombe kwa Euro 107,000 kutoka AS Cannes na mgawo wa Simba unapaswa kuwa Euro 43,000 ambazo ni asilimia 40 ya kiwango hicho. 
    Zacharia Hans Poppe kulia ameonya kiongozi yeyote wa Simba SC asipokee fedha za Kapombe kutoka Azam, bali malipo yafanywe na AS Cannes

    Poppe amesema kwamba akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili yeye ndiye aliyeshughulikia suala zima la Kapombe kwenda AS Cannes na ndiye anayejua kila kitu, hivyo anashangaa kwa sasa watu wengine wanaliingilia kati.
    “Katika uongozi huu huu ambao unamaliza muda wake, mimi ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili  na ndiye niliyeshughulikia suala la Kapombe, sasa iweje leo wakati wa malipo mambo yaende kimya kimya?,”alihoji. 
    Poppe amesema Simba SC inahitaji fedha kwa ajili ya kufanyia usajili na ametaka fedha hizo ziwasilishwe katika utaratibu na ziingie kwenye klabu.
    Maisha Azam; Shomary Kapombe kulia

    “Taratibu zifuatwe, Azam hawawezi kutulipa sisi, wao walipe Cannes, na Cannes watulipe sisi asilimia 40 yetu,”alisema.
    Tayari Kapombe amesaini Mkataba wa miaka mitatu na Azam FC baada ya kugoma kuendelea kuichezea AS Cannes Novemba mwaka jana.
    AS Cannes ilimchukua bure Kapombe kutoka Simba akiwa amebakiza Mkataba wa mwaka mmoja kwa makubalino ya kumuendeleza na kumuuza Ulaya.
    Klabu hiyo ya Daraja la Nne Ufaransa ilimsainisha Kapombe Mkatabva wa miaka minne, lakini baada ya kugoma kurejea Ulaya ameuzwa Azam FC. Azam bado hawajaweka wazi kiwango halisi walichotoa Cannes kumnunua Kapombe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FEDHA ZA KAPOMBE ZAZUA BALAA MSIMBAZI, HANS POPPE ASEMA AZAM HAWAHUSIKI, MALIPO YAFANYWE NA AS CANNES Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top