• HABARI MPYA

    Tuesday, April 09, 2013

    YANGA WALIMWA FAINI KWA MCHEZO MBAYA LIGI KUU

    Mabingwa watarajiwa; Yanga SC wamelimwa faini

    Na Boniface Wambura
    KLABU ya Yanga na Kocha Msaidizi wa timu ya Toto Africans, Athuman Bilali wamepigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja kutokana na makosa mbalimbali katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea nchini.
    Adhabu hizo zimetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Jumapili (Aprili 7 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za waamuzi na makamishna kwa michezo namba 108 hadi 171.
    Yanga imepigwa faini hiyo baada ya kupata kadi tano za njano katika mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Februari 7 mwaka huu. Vilevile Kagera Sugar imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) dhidi ya African Lyon iliyochezwa mjini Bukoba, Februari 23 mwaka huu.
    Naye Kocha Bilali amepigwa faini hiyo na kufungiwa mechi tatu za ligi hiyo kwa kumshambulia kwa maneno kocha wa timu pinzani, hali iliyosababisha mwamuzi amtoe kwenye benchi la wachezaji. Alifanya tukio hilo kwenye mechi kati ya Toto Africans na Tanzania Prisons iliyochezwa Aprili 3 mwaka huu jijini Mwanza.
    African Lyon na Simba zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa kushindwa kuchezesha timu zao za U20 kwenye mechi za utangulizi wakati zilipocheza na Oljoro JKT na Coastal Union, Machi mwaka huu kwenye viwanja vya Azam Complex na Uwanja wa Taifa.
    Suala la Meneja wa Coastal Union, Akida Manchai kumshambulia kwa maneno yasiyo ya kiungwana Makamu Mwenyekiti wake Steven Mnguto baada ya kwenye mechi kati ya African Lyon na Coastal Union iliyochezwa Machi 30 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex limepelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
    Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom.
    Wakati huo huo: Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho, wakati Polisi Morogoro itakapopambana na Ruvu Shooting katika mchezo ambao, matokeo yake yanatarajiwa kutoa mwanga kama Polisi inaweza kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.
    Timu hiyo itakuwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika mechi hiyo itakayochezeshwa na Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Ephrony Ndissa wa Arusha.
    Polisi Morogoro inayonolewa na Mohamed ‘Adolph’ Rishard inakamata nafasi ya mwisho ikiwa na pointi 18 tu na imebakiza mechi tatu dhidi ya Simba, Kagera Sugar na Coastal Union.
    Mechi nyingine za kesho ni kati ya Tanzania Prisons iliyo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 20 dhidi ya Mgambo Shooting. Mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam ndiye atakayechezesha mechi hiyo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. Mgambo ina pointi 24 na iko katika nafasi ya tisa.
    Mwamuzi Said Ndege wa Dar es Salaam atachezesha mechi kati ya wenyeji Mtibwa Sugar na Toto Africans itakayofanyika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Toto Africans ya Kocha John Tegete ina pointi 21 ikiwa nafasi ya 11 wakati Mtibwa Sugar iko nafasi ya tano na pointi zake 32.
    Ligi hiyo itaendelea keshokutwa (Aprili 11 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Azam na African Lyon itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex.
    Katika hatua nyingine, Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imezipongeza timu za Ashanti United ya Dar es Salaam, Mbeya City ya Mbeya na Rhino Rangers ya Tabora kwa kupanda Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2013/20114).
    Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Wallace Karia amezitaka timu hizo kufanya maandalizi ya kutosha ili ziweze kushindana katika VPL ikiwemo kutimiza masharti ya kuwa klabu za Ligi Kuu.
    Moja ya masharti ya klabu zenye hadhi ya Ligi Kuu ni kuwa na timu ya pili (U20) ambayo itakuwa na inacheza mechi za utangulizi kwenye uwanja wa nyumbani kila timu ya wakubwa inapocheza.
    Mbali ya kuthibitisha timu hizo tatu kupanda daraja, pia Kamati ya Ligi imethibitisha rasmi timu tatu zilizoshuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa katika mkoa husika. Timu zilizoshuka kutoka Daraja la Kwanza (FDL) ni Small Kids ya Rukwa kutoka kundi A.
    Kundi B timu iliyoshuka ni Moro United ya Dar es Salaam wakati Morani FC ya Manyara yenyewe imeporomoka kutoka kundi C.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WALIMWA FAINI KWA MCHEZO MBAYA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top