• HABARI MPYA

    Tuesday, April 09, 2013

    MWINYI KAZIMOTO NA FELIX FUNZU WASAMEHEWA RASMI, WAANZA KAZI TENA LEO SIMBA SC

    Amerudi; Mwinyi anaanza mazoezi leo

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIUNGO Mwinyi Kazimoto Mwitula na mshambuliaji Mzambia, Felix Mumba Sunzu Jr. wanatarajiwa kuanza mazoezi leo jioni baada ya kusimamishwa kwa kipindi cha wiki mbili kutokana na utovu wa nidhamu.  
    Hiyo inafuatia kikao cha jana usiku baina ya uongozi wa Simba SC, benchi la ufundi na wachezaji hao kufikia suluhu ya tatizo lililokuwapo.
    “Kikao cha jana kilikuwa kizito sana, Mwalimu (Patrick Liewig) alikuwa ana msimamo wa kuendelea kutowahitaji wachezaji wao, lakini viongozi walitumia busara kuwaombea msamaha, hadi akalainika na kuwakubali,”amesema leo asubuhi, Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga.
    Mwinyi na Sunzu ni kati ya wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza walioenguliwa kwenye programu ya kocha huyo Mfaransa, kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wao mzima wa kitabia.
    Wengine ni mabeki Juma Nyosso, Paul Ngalema, Amir Maftah, Komalbil Keita, viungo Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Haruna Moshi ‘Boban’ na mshambuliaji Abdallah Juma. 
    Nyota hao wote wamekosa mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu, dhidi ya Coastal Union ya Tanga, Kagera Sugar ya Bukoba na Toto African ya Mwanza, ambazo Simba ilishinda moja, sare moja na kufungwa moja.
    Kwa sasa, kikosi cha Simba SC kinaundwa na wachezaji wengi wa kikosi cha pili, waliokuwa wanaongezewa nguvu na wachache wa kikosi cha kwanza akina Juma Kaseja, Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Shomary Kapombe, Amri Kiemba, Mrisho Ngassa, Kiggi Makassy, Salim Kinje na sasa Mwinyi na Sunzu wanaongezeka.   
    Kwa sasa Simba SC, ambao ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu wanajifua vikali, kujiandaa na mchezo wake ujao wa ligi hiyo dhidi ya Azam FC Jumamosi wiki hii.
    Simba SC ipo katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 35, nyuma ya Kagera Sugar yenye pointi 37, Azam FC 43 na Yanga iliyo kileleni kwa pointi zake 49.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MWINYI KAZIMOTO NA FELIX FUNZU WASAMEHEWA RASMI, WAANZA KAZI TENA LEO SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top