Na Prince Akbar
![]() |
| Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano wa SBL, Teddy Mapunda kulia, akijadiliana na jambo na Mkurugenzi wake, Richard Wells jana |
KATIKA ukumbi uliopambwa vema- taa zenye mwanga mzuri wa
rangi tofauti na mpangilio mzuri wa viti na meza sambamba na majukwaa mawili-
moja la burudani na lingine la kutolea tuzo- shughuli ya Utoaji wa Tuzo za Wanamichezo
Bora Tanzania kwa mwaka jana, ilifana jana.
Unaweza kusema nini zaidi ya shukrani kwa Kampuni ya Bia ya Serengeti
(SBL), iliyodhamini tuzo hizo, zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania, TASWA?
Hakika SBL wanastahili pongezi. Tena sana, kwa kudhamini
tuzo hizi, ambazo lengo lake ni kutambua na kuthamini mchango wa wanamichezo wa
taifa hili, ambao kwa hakika wanastahili heshima ambayo pengine kwa sasa hawaipati
kwa kiwango kinachotakiwa.
SBL iliyotumia kiasi cha Sh. Milioni 150 kudhamini tuzo
hizo, imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia michezo na sekta nyingine
mbalimbali za kitaaluma na kijamii kwa ujumla nchini.
Hapana shaka ni sera nzuri, chini ya uongozi bora wa kampuni
hiyo, chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya SBL, Jaji Mark Bomani, Mkurugenzi wake,
Richard Wells, Mkurugenzi wa Masoko, Ephraim Mafuru, Mkurugenzi wa Mawasiliano
na Mahusiano wa kampuni hiyo, Teddy Mapunda.
Lakini pia huwezi kuacha kutoa pongezi kwa wa TASWA, chini ya
Mwenyekiti wake Juma Abbas Pinto na Katibu Mkuu wake, Amir Ally Mhando kwa
utendaji wao mzuri, uliozifanya tuzo hizo sasa zirejeshe heshima yake.
Katika usiku huo, ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee,
katikati ya Jiji la Das es Salaam, mwanasoka chipukizi nchini, Shomary Kapombe
aliibuka kinara, baada ya kutwaa tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Mwaka na
kuzawadiwa kitita cha Sh. Milioni 12.
Awali, Kapombe anayechezea klabu bingwa ya Tanzania, Simba
SC, alizawadiwa Sh. Milioni 1 kwa kutwaa tuzo nyingine ya Mwanamichezo Bora Chipukizi
Tanzania- ingawa wengine walihoji kwa nini hata tuzo ya Mwanasoka Bora aliyoshinda
beki Aggrey Morris wa Azam, FC, asiipate yeye pia?
Wanaweza kuwa wana hoja wenye mtazamo huo- kwani sababu
Kapombe kama ni Mwanamichezo Bora Tanzania, basi lazima awe bora kwanza kwenye
mchezo anaoucheza.
Lakini hili si suala zito sana, kwa sababu Kamati iliyopewa
jukumu la kufanya mchakato huu ilikuwa huru na imefanya kulingana na taratibu
ilizojiwekea, chini ya Mwenyekiti wake, Mwandishi wa Habari za michezo mwandamizi
Tanzania, Masoud Saanan.
![]() |
| Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, Eiphraim Mafuru kulia akikabidhi tuzo |
![]() |
| Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto kulia |
Pongezi zaidi kwa TASWA kwa kupanua wigo wa tuzo- na sasa
hadi Mwanasoka wa Tanzania anayecheza nje anazawadiwa na jana imeshuhudiwa
Mbwana Ally Samatta wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC) akishinda tuzo hiyo.
Yote kwa sababu ya fungu la kutosha kutoka kwa wadhamini,
SBL, ambao wamekuwa wepesi mno kupiga jeki shughuli mbalimbali za michezo nchini
zinapokwama.
Shoo ya tuzo ilifana. Bendi ya Extra Bongo chini ya uongozi
wake Ally Choky Rwambo ilifanya vizuri katika jukwaa lililokuwa upande wa kushoto
wa ukumbi. Wane Star naye alifanya vema kwa ngoma zake za asili.
Waongoza shughuli (ma MC) Gadna Habash na Ephraim Kibonde
walifanya vema kwa upande wao- sauti zao ni maarufu na zinapendwa sana. Walitumia
uzoefu wao kuongoza vema shughuli hiyo, ambayo mgeni wake rasmi alikuwa rais
Mstaafu wa awamu ya Pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi.
Mzee Mwinyi ni kiongozi ambaye anapendwa sana na Watanzania
kutokana na kile ambacho unaweza kukiita hekima na busara aliyonayo na jana japokuwa
alipanda jukwaani kuhutubia wakati ‘muda umeenda sana’ watu walivumilia maelezo
yake marefu akitoa nasaha za msingi katika sekta ya michezo.
Alisema mengi Mzee Mwinyi, lakini kikubwa alisistiza
maandalizi mazuri kwa timu zetu kabla ya kuingia kwenye mshindano ili kuepuka
kufanya vibaya. Mzee Mwinyi, aliyemrithi marehemu Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere kiti cha urais wa Tanzania mwaka 1985 kabla ya kumuachia Benjamin
William Mkapa miaka 10 baadaye, aliwataka wanamichezo walioshinda tuzo hizo,
kutobweteka, badala yake kuongeza juhudi ili kusaka mafanikio zaidi.
Ulikuwa usiku mzuri jana ndani ya Diamond Jubilee na asanté sana
SBL. Hongera TASWA.
![]() |
| Mzee Mwinyi kulia akimkabidhi tuzo Kapombe kushoto kabisa jana. Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa Simba Sc, Geoffrey Nyange 'Kaburu' na Mkurugenzi wa SBL. Richard Wells. |






.png)
0 comments:
Post a Comment