• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 23, 2012

  MANCINI AMPA WIKI MBILI TEVEZ

  Carlos Tevez
  MANCHESTER, England
  MSHAMBULIAJI wa kiargentina, Carlos Tevez anaweza kurejea kuichezea Manchester City baada ya wiki zisizozidi mbili.
  Kocha wa City,Roberto Mancini amesema kwamba ameukubali msamaha wa Tevez kwa kosa alilofanya kukataa kuinuka kupasha misuli moto Septemba, mwaka jana katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich.
  Mancini alisema anajiandaa kumrudisha kikosini Muargentina huyo.
  Mancini alisema; “Labda atahitaji wiki mbili au tatu ili kuwa katika kiwango kizuri, kama yuko sawa, atacheza.” Mancini alisema leo atakutana na mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye hivi karibuni amerejea kutoka mapumzikoya miezi mitatu Amerika Kusini bila ruhusa ya klabhu yake..
  Mapema jana,  Tevez aliomba radhi kwa tabia yake isiyofaa hivi majuzi, na iliyoanza tangu alipogombana na meneja Roberto Mancini mwezi Septemba.
  “Ningelipenda kuomba msamaha kwa dhati na pasipo kikwazo chochote kwa kila mtu, na kwa yoyote yule niliyemkosea kwa vitendo vyangu ikiwa nimemuudhi”, alielezea Tevez kupitia taarifa. Wakati huo huo Tevez amefutilia mbali malalamiko aliyokuwa amewasilisha rasmi dhidi ya klabu ya Man City.
  “Nia yangu sasa ni kuhusika zaidi katika kuichezea soka klabu ya Manchester City”, alisisitiza.
  Baada ya kushindwa kujiunga na AC Milan ya Italia kama ilivyotazamiwa wakati wa usajili wa mwezi Januari, Tevez bila shaka alikuwa na uamuzi mgumu wa kuamua iwapo aendelee kupumzika na akicheza golf huko Argentina, ama arudi tena mjini Manchester na kujaribu kupigania nafasi yake katika timu yake.
  Kuna uwezekano bado wa Tevez kuhama wakati wa msimu wa joto, lakini angalau inaelekea kwa hivi sasa uwanja wa Etihad umetulia, baada ya sokomoko iliyozushwa na mchezaji huyo.
  Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina hajawahi kuichezea City tangu mwezi Novemba, wakati meneja Roberto Mancini anadai alikataa kuingia uwanjani kama mchezaji wa zamu, na hatimaye timu kushindwa na Bayern Munich ugenini magoli 2-0 katika mechi ya klabu bingwa mwezi Septemba.
  Tevez anadai kulikuwa na hali ya sintofahamu na mkorogano wa lugha, na akaeleweka vibaya.
  Moja kwa moja baada ya ugomvi huo, Mancini alisema Tevez “amekwisha” kama mchezaji wa City, lakini baadaye alielezea kuna uwezekano wa mchezaji huyo kukaribishwa tena katika timu, ikiwa ataomba msamaha.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MANCINI AMPA WIKI MBILI TEVEZ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top