• HABARI MPYA

  Friday, February 24, 2012

  SIMBA WAANZIA GYM KUIKUSANYIA NGUVU KIYOVU

  VINARA wa Ligi Kuu, Simba wameanza kujifua kwa mazoezi ya gym jana asubuhi kujiwinda na mechi yao ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Kiyovu ya Rwanda pamoja na mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
  Katika mazoezi hayo wachezaji nyota wa Zambia, Felix Sunzu, kiungo Haruna Moshi 'Boban' na Ulimboka Mwakigwe wakikosa mazoezi hayo.
  Ilishuhudiwa timu hiyo ikijifua katika gym ya Oil Com Chang'ombe huku wachezaji 17, wakiwa chini ya kocha Milovan Cirkovic.
  Milovan alisema ameanza na mazoezi ya gym ili kuwaamsha wachezaji waliokuwa kwenye mapumziko kabla ya kuanza kwa mazoezi ya uwanjani.
  ''Kama unavyoona maandalizi ni mazuri, tumeanza na gym baada ya mapumziko ya muda mrefu, naamini itasaidia kuwaamusha na kuwajenga wawe na nguvu baada ya mapumziko,''alisema Milovan.
  Hata hivyo, majeruhi waliokuwa wakikisumbua kikosi hicho wamepona Amir Maftah alifanya mazoezi na Victor Costa alikuwa akifanya mazoezi mepesi.
  Daktari wa timu, Cosmas Kapinga amesema; ''Sasa hakuna majeruhi katika kikosi chetu, hao wote wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali ni matatizo madogo tu.''
  Kikosi cha Simba kinataraji kushuka dimbani kesho kuvaana na Azam Fc katika mchezo wa kirafiki utakaochezwa kwenye uwanja wa Chamazi ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao.
  Akizungumza jana Katibu mkuu wa Simba Evodius Mtawala alisema mbali na mchezo huo wanaamini mechi kati ya Taifa Stars na Msumbiji pia itakuwa kipimo tosha kwa wachezaji wao kabla ya kuivaa Kiyovu siku mbili baadae.
  Simba itaingia uwanjani kuivaa Azam bila ya nyota wake walioitwa kwenye kikosi cha Stars, imefufua matumaini baada ya majeruhi wake Amir Maftah, Ulimboka Mwakingwe pamoja na Haruna Moshi kupona na kucheza katika pambano hilo.
  Mtawala alisema timu hiyo inaendelea na mazoezi chini ya kocha Milovan tayari kwa pambano hilo na wamepani kuendeleza heshima nyumbani na kuhakikisha wanatoka na ushindi.
  "Jumamosi hii tutacheza na Azam asubuhi katika pambano la kirafiki, tunaendelea vyema na maandalizi ya mchezo wetu wa marudio ambao utachezwa hapa nyumbani wikiijayo na kila kitu kinakwenda vizuri,"alisema Mtawala.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA WAANZIA GYM KUIKUSANYIA NGUVU KIYOVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top