• HABARI MPYA

  Saturday, February 25, 2012

  MAREFA WA KIARABU KUCHEZEASHA ZAMALEK NA YANGA JESHINI

  WAKATI kocha wa Yanga, Mserbia Kostadin Bozidar Papic amelishutumu Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kudhoofisha maandalizi yao ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek, shirikisho hilo limetuma pia taarifa ya kuwakata maini zaidi wana Jangwani hao. CAF imetuma taarifa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikitaja marefa watakaochezesha mchezo huo wa marudiano, Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa, ambao utachezwa mwishoni mwa wiki ijayo mjini Cairo, wote wakiwa ni kutoka Kaskazini mwa Afrika.
  Hao ni Jihed Redouane, Rouani Bouazza na Bekkali Mimoun kutoka Morocco wakati refa wa akiba ni Gihed Greisha wa pale pale Misri na Kamisaa ni Ben Khadiga wa Tunisia.
  Aidha, CAF wameitaka TFF iwataarifu Yanga kwenda na msafara wa watu wasiozidi 40 katika mchezo huo wa marudiano, Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa, ambao utachezwa mwishoni mwa wiki ijayo mjini Cairo.
  Ofisa Habari wa TFF, Boniphace Wambura Mgoyo, alisema jana kwamba CAF imetaka idadi hiyo ndogo tu kutokana na maombi ya Wamisri, kwa vile Zamalek inakabiliwa na adhabu ya kucheza mechi hiyo bila mashabiki.
  Zamalek inakabiliwa na adhabu ya kucheza mechi mbili za nyumbani za michuano hiyo bila mashabiki baada ya Aprili 20, mwaka jana Bodi ya Nidhamu ya CAF iliyokutana jijini Johannesburg, Afrika Kusini kutoa hukumu hiyo.
  Mechi dhidi ya Yanga ndiyo itakayokuwa ya kwanza kwa Zamalek kuanza kutumikia adhabu hiyo iliyotakana na mashabiki wake kufanya fujo kwenye mechi ya michuano hiyo mwaka jana, ilipocheza dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
  Hivyo kila timu (Yanga na Zamalek) katika mechi hiyo inatakiwa kuwa na wachezaji ambao wana leseni za CAF kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa 2012. Pia benchi la ufundi katika kila timu linatakiwa kuwa na watu watano.
  Kwa klabu zote mbili, kila moja imeruhusiwa kuingia na wajumbe wake wa Kamati ya Utendaji wasiozidi kumi. Mbali ya klabu hizo mbili, wengine waliotajwa kuruhusiwa kuingia uwanjani ni vijana 20 watakaofanya kazi ya kuokota mipira (ball-boys).
  Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo, Papic alisema kwamba hadi sasa hawana taarifa rasmi kutoka CAF juu ya siku na mahali ambako mechi hiyo ya marudiano itachezwa, hali ambayo alisema inadhoofisha maandalizi yao.
  Papic alisema kwamba kimsingi wanatakiwa kuondoka Dar es Salaam Alhamisi, lakini hadi jana walikuwa hawajashughulikia viza wala tiketi, kwa sababu hawajui wanakwenda kucheza nchi gani kutokana na mkanganyiko uliokuwapo awali kwamba mechi inaweza kuchezwa Sudan.
  “Siwezi kusema chochote kwa sasa, siwezi kusema tuko vizuri, lakini naweza kusema hatuko vibaya, CAF wanatuchanganya sana. Tulitakiwa kujua mapema tunacheza wapi,” alisema.
  Japokuwa Yanga wanadai hawajapata taarifa kutoka CAF, lakini Msemaji wa Zamalek, Ali Aboul-Naga Said, wiki hii amekaririwa akisema kwamba wamependekeza mechi hiyo ichezwe katika Uwanja wa Arab Contractors, unaomilikiwa na jeshi la nchi hiyo uliopo Cairo, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 22,000.
  Utata kuhusu wapi itakapochezwa mechi hiyo ya marudiano ulitokana na vurugu zilizotokea Misri kwenye uwanja wa Port Said na kusababisha watu 74 kupoteza maisha, wakati wa mechi ya Ligi Kuu nchini humo kati ya Ahly dhidi ya Al Masry.
  Kutokana na hali hiyo, Zamalek walisema kama serikali itashikilia uamuzi wa kuzuia mechi za soka kuchezwa nchini Misri, watalazimika kucheza mechi yao ya marudiano na Yanga nje katika nchi ya Algeria au Sudan.
  “Tunatumaini tutafahamu vizuri kuhusu hali ya usalama hapa na kama serikali itatupa ruhusu ya kucheza mchezo wetu hapa au la,” alisema msemaji wa Zamalek, Ali Aboul-Naga Said.
  Zamalek imepokea maombi kutoka klabu ya Algeria, ES Setif na Hilal ya Sudan kuwa wenyeji wa miamba hiyo ya Cairo inayopewa nafasi ya kusonga mbele baada ya kupata sare ya 1-1 ugenini Jumamosi iliyopita.
  Tayari Serikali ya kijeshi ya Misri imetoa ruhusa kwa Zamalek kucheza mechi hiyo nyumbani kwenye Uwanja huo wa chuo cha jeshi uliojengwa mwaka 1989 kwa lengo la kutumika kwa michezo ya majeshi pekee, ukiwa kwenye Mtaa wa Onouba, kaskazini mwa jiji la Cairo, umbali wa maili 7 kutoka uwanja wa kimataifa wa Cairo.
  Katika mchezo huo, Yanga wanatakiwa kulazimisha ushindi ugenini, baada ya Jumamosi iliyopita kulazimishwa sare ya kufungana 1-1 na mabingwa mara tano Afrika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAREFA WA KIARABU KUCHEZEASHA ZAMALEK NA YANGA JESHINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top