• HABARI MPYA

  Tuesday, February 21, 2012

  STARS NA DRC KUPIGWA JIONI KABISA

  MCHEZO wa kirafiki wa kimataifa kati ya timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itakayochezwa Alhamisi wiki hii itaanza saa 11 jioni. 
  Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, Boniface Wambura alisema jana kuwa hatua hiyo inatokana na kutaka kuwapa nafasi mashabiki wengi ambao ni wafanyakazi kuweza kupata muda wa kuwahi mchezo huo. “
  Kwa vile Februari 23 mwaka huu ni siku ya kazi ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi kushuhudia pambano hilo la kimataifa, mechi hiyo itaanza saa 11 kamili jioni,” alisema Wambura.  
  Kwa kawaida mechi nyingi huanza wakati wa alasiri na mara chache zimekuwa zikifanyika kuanzia saa moja usiku. 
  Wakati huohuo, Wambura alisema kiingilio chini kwa ajili ya mechi hiyo kitakuwa Sh 2,000 kwa viti vya kijani na bluu, ambapo viti vya rangi ya chungwa kiingilio ni Sh 5,000, VIP C itakuwa Sh 7,000 wakati VIP B tiketi zitauzwa kwa Sh 10,000. Kiingilio kwa viti vya VIP A kitakuwa Sh 15,000.  
  Taifa Stars inayofundishwa na Jan Poulsen iliingia kambini jana, ambapo DRC ambayo iko chini ya kocha Claude Le Roy inatarajia kutua nchini leo. 
  Taifa Stars na DRC zinatumia mechi hiyo kunoa wachezaji wao kabla ya mechi zao za mchujo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.  
  Katika raundi hiyo ya awali ambayo mechi zake zitachezwa Februari 29 mwaka huu, Stars itaanzia nyumbani dhidi ya Msumbiji wakati DRC inaanzia ugenini dhidi ya Shelisheli.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: STARS NA DRC KUPIGWA JIONI KABISA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top