• HABARI MPYA

  Saturday, February 25, 2012

  POULSEN: UKUTA TAFA STARS SAFI SANA

  KOCHA wa timu ya Taifa Stars, Jan Poulsen amesema amefurahishwa na safu ya ulinzi ilivyocheza dhidi ya DR Congo, isipokuwa ana kazi ya ziada kujenga safu ya ushambuliaji.
  "Bado tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunatengeneza timu ambayo itakuwa imara idara zote, na siyo kwa safu ya ulinzi pekee," alisema Poulsen.
  "Hatuwezi kucheza vizuri katika safu ya ulinzi lakini tukashindwa kufunga mabao, hili haliwezekani kabisa tunahitaji ushindi kwenye michezo yetu," alisisitiza.
  Poulsen alisema anashangazwa kuona washambuliaji wake wakicheza tofauti na maelekezo, lakini kwenye mazoezi wanaonekana kufanya vile anavyofundisha.
  "Hivi sasa safu ya ulinzi ya Taifa Stars ni nzuri kwa sababu timu nyingi duniani huanza kuundwa kwa kujengwa safu hiyo ambayo inapaswa kuwa imara zaidi."
  Safu ya ulinzi ya Taifa Stars katika mechi hiyo iliundwa na Agrrey Morris, Juma Nyoso, Shadrack Nsajigwa na Stephano Mwasika.
  Taifa Stars katika mechi hiyo kwenye vipindi vyote walicheza mchezo wa kulinda zaidi kuliko kushambulia, isipokuwa waliweza kupiga pasi kutoka nyuma hadi mbele kushambulia.
  Tatizo kubwa lililoonekana kwa Stars ni kujificha na kusahau kufungua na kuomba pasi wakati mwenzao anapokuwa na mpira hucheza vizuri na kumiliki muda mrefu.
  Ni wachezaji watano wa Stars, Mrisho Ngasa, John Boko, Abdi Kassim, Mwinyi Kazimoto na Jonas Mkude walijaribu kupiga mashuti katika lango la DR Congo bila kuwa na shabaha.
  Taifa Stars walikuwa wakitegemea kutengeneza mashambulizi yake kupitia pembeni mwa uwanja kwa kuwatumia Ngassa na Javu kabla ya kuingia kwa Nsa Job na Uhuru Seleiman.
  Kocha Poulsen katika mechi hiyo aliwapa nafasi wachezaji wawili vijana katika nafasi ya kiungo, Salum Abubakar na Jonas Gerard ambao walionyesha uhai pamoja na upya wao kwenye kikosi hicho.
  Mechi hiyo ilikuwa sehemu ya maandalizi kwa Stars kuelekea mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi Msumbiji wiki ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: POULSEN: UKUTA TAFA STARS SAFI SANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top