• HABARI MPYA

  Tuesday, February 21, 2012

  GUMBO, BERKO WAREJEA KUIZUIA ZAMALEK AFRIKA

  MAJERUHI waliokuwa wanaikabili timu ya Yanga sasa wako katika hali nzuri ya kuichezea timu hiyo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.
  Imeelezwa. Majeruhi hao ni kipa chaguo la kwanza, Yaw Berko, viungo Nurdin Bakari, Godfrey Bonny, Rashidi Gumbo na Salum Telela, ambapo wote hali zao zimeimarika na wako tayari kuendelea kuichezea tena timu hiyo. 
  Akizungumza na gazeti hili jana, daktari wa Yanga Nassoro Matuzya alisema Berko alikuwa akisumbuliwa na goti na alishaanza mazoezi mepesi na leo ataendelea na programu maalumu ya kuimarisha afya yake. 
  Matuzya alisema Bakari aliyevunjika kidole akiwa tayari ameondolewa plasta ngumu na kwamba anaweza kuanza mazoezi, huku, Bonny aliyekuwa akisumbuliwa zaidi na malaria kwa muda mrefu na nyama za paja naye yuko vizuri. 
  Aliongeza kuwa kiungo mchezeshaji Gumbo ambaye alikuwa anasumbuliwa na goti naye yuko vizuri na ameshamkabidhi kwa kocha wa timu hiyo Kostadin Papic na kwamba yeye ndio mwenye uamuzi wa mwisho wa kumtumia, huku Telela aliyeumia kifundo cha mguu akiwa anaendelea vizuri na mpaka kufikia Ijumaa wiki hii ataweza kuanza mazoezi na timu hiyo. 
  Kurejea kwa nyota hao waliokosa mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek ambapo walilazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani ni faraja kwa Papic ambapo sasa atakuwa na uwanja mpana wa kuchagua wachezaji wa kuichezea timu hiyo. 
  Papic mara kadhaa amenukuliwa akilalamikia kuongezeka kwa majeruhi, kiasi cha kuharibu mipango yake ya kuiandaa timu hiyo kwa ajili ya mechi mbalimbali za Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa. Watarudiana na Zamalek jijini Cairo mwishoni mwa wiki ijayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GUMBO, BERKO WAREJEA KUIZUIA ZAMALEK AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top