• HABARI MPYA

  Saturday, February 25, 2012

  KASHESHE LA MAPATO YANGA NA ZAMALEK

  SAKATA la mapato ya mechi ya Yanga, limechukua sura mpya baada ya jana Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano ya klabu hiyo, Mohamed Bhinda kuamua kupasua jipu na kuweka wazi mlolongo mzima wa mapato hayo ya mechi dhidi ya Zamalek ya Misri.
  Katika mechi hiyo ya sare ya bao 1-1, Ligi ya Mabingwa Soka Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wiki moja iliyopita, Sh286milioni zilipatikana.
  Akizungumza jana, Bhinda alisema ameamua kuweka mambo wazi ili Wanayanga waujue ukweli halisi na wakati huohuo yeye mwenyewe kujisafisha na tuhuma anazopewa kuhujumu Sh20milioni za mapato ya mechi hiyo.
  Bhinda amesema hastahili kubeba mzigo wa lawama hizo na badala yake amewataja, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga na Katibu Mkuu, Selestine Mwesigwa ndiyo wanaopaswa kuulizwa.
  Alisema, kwa mujibu wa mkataba na kampuni ya Prime Time ambao Nchunga ndiye aliyesaini kwa upande wa Yanga, uliitaka klabu hiyo isihusike na jambo lolote kwa vile kila kitu kitasimamiwa na Prime Time," alisema Bhinda.
  Kwa mujibu wa Bhinda, kampuni hiyo ilikuwa na jukumu la kusimamia uuzaji wa tiketi, matangazo na kupata gawio la asilimia 20 ya mapato yote ya mchezo huo.
  Akifafanua zaidi alisema, yeye binafsi aliingia kwenye jukumu la kuuza tiketi kwa makubaliano na Prime Time baada ya utaratibu wa kuuza tiketi mapema kushindika hali iliyoleta vurugu kwa mashabiki.
  "Siku ile ambayo ilitangazwa tiketi zingeanza kuuzwa Ijumaa asubuhi, zoezi hilo lilichelewa na badala yake zikauzwa kuanzia saa nane mchana.
  "Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa Prime Time (Joseph Kusaga) aliniomba nisaidie zoezi hilo kwa mkataba katika vituo vya Temeke Mwembe Yanga, Mbagala, Veta na Buguruni ambapo baada ya mauzo zilipatikana Sh71milioni.
  Bhinda alisema alizikabidhi fedha hizo za mauzo ya tiketi Prime Time, lakini katika hali ambayo hailewi imekuja vipi, ameshangazwa kuhusishwa na upotevu wa Sh20milioni.
  "Hizi 20milioni nazohusishwa kuchukua zimetoka wapi? Mimi nilikabidhi pesa zote kwa wahusika na baada ya kuzihesabu waliridhika kulingana na idadi ya tiketi nilizouza," alisema Bhinda na kuongeza kwamba alilipwa Sh2milioni kwa kazi hiyo.
  Hata hivyo Bhinda hakutaka kuzungumzia kwa undani mchanganuo wa mpato hayo kwamadai kuwa wenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Mwenyekiti Nchunga na Katibu Selestine Mwesigwa.
  "Kila kitu anajua mwenyekiti (Nchunga) yeye na katibu (Mwesigwa) ndiyo walikwenda kusaini mkataba. Hawa wanafahamu kila kitu, kama kuna jambo la kuulizwa basi wao ndio wanastahili," alisema Bhinda.
  Mchanganuo zote kwenye mchezo huo ni Sh286,695,000. Inadaiwa kuwa, baada ya makato yote Yanga ilibaki na kiasi cha Sh88milioni.
  Akizungumzia suala hilo, katibu wa Yanga Selestine Mwesigwa alisema: "Bhinda siyo muajiriwa wa Yanga, yeye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji, yeye ni kama bosi wangu, siwezi kuongeza zaidi."
  Aliongeza: "Aliyoongea (Bhinda) ni masuala yake binafsi, ana uhuru wa kufanya anachotaka, kuingia mkataba na yeyote. Alichoongea tunapaswa kukiheshimu. Kila jambo lina ukweli," alisema zaidi Mwesigwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KASHESHE LA MAPATO YANGA NA ZAMALEK Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top