• HABARI MPYA

    Wednesday, October 19, 2016

    SIMBA NA KLABU YA NDUSHA WAFIKISHANA FIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SUALA la utata wa kimkataba wa kiungo mpya wa Simba, Chichi Mussa Ndusha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limefikishwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ili kupatiwa ufumbuzi.
    Simba SC imemsajili mchezaji huyo msimu huu, lakini imeshindwa kuanza kumtumia katika mechi za mashindano kutokana na klabu aliyotokea, FC Renaissance kuweka ngumu.
    Na klabu hiyo ya DRC inadai bado ina Mkataba naye hivyo imelizuia Shirikisho la Soka DRC kutuma Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) aanze maisha mpya Dar es Salaam.
    Simba imefungua kesi FIFA kwa ajili ya kiungo Chichi Mussa Ndusha kutoka DRC 

    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas Mapunda ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo kwamba, kwa sababu hiyo, Simba SC imeamua kufungua kesi FIFA, ikipeleka vielelezo vya kuonyesha mchezaji huyo hana Mkataba na FC Renaissance.
    “Kwa kweli niseme tu mustakabali wa mchezaji huyo hadi sasa ni tata. Tunachosubiri ni hiyo Kamati ya FIFA kuketi na kupitia mikataba hiyo na kutoa maamuzi,”amesema Lucas.   
    Ndusha ni kati ya wachezaji wapya watano wa kigeni waliosajiliwa msimu huu, wengine wakiwa ni Janvier Bokungu kutoka DRC pia, Method Mwanjali kutoka Zimbabwe, Frederick Blagnon kutoka Ivory Coast na Laudit Mavugo kutoka Burundi. 
    Watano hao wote wapya wameungana na wawili kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast na beki Mganda Juuko Murshid waliobaki kutoka kikosi chaa msimu uliopita baada ya kuachwa kwa beki Mrundi Emery Nimubona, kiungo Mzimbabwe, Justice Majabvi na washambuliaji Mganda Hamisi Kiiza, Pape Ndaw kutoka Senegal na Mkenya Paul Kiongera.  
    Wakati huo huo: Simba SC inaendelea na maandalizi ya mchezo wake wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC ya Mwanza na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog ana matumaini makubwa ya kuendeleza wimbi la ushindi.
    Simba SC inagongoza Ligi Kuu sasa ikiwa imejikusanyia pointi 23 baada ya kucheza mechi tisa, ikifuatiwa na Stand United ya Shinyanga yenye pointi 20 za mechi 10, wakati mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 15 za mechi nane ni wa tatu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA KLABU YA NDUSHA WAFIKISHANA FIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top