• HABARI MPYA

    Monday, February 15, 2016

    AYA 15 ZA SAID MDOE: MUZIKI WA DANSI BADO KUZIKWA TU, UMEKWISHAUAWA!

    IPO imani kwamba baadhi ya  watangazaji hawautaki muziki wa dansi wakiamini kuwa ni muziki ambao hautakiwi tena na mashabiki. “Watu hawautaki tena muziki wa dansi …muziki wa dansi umekufa,” 
    Hiyo ni mitazamo yao na sitaki kuwa hakimu kwenye hisia zao – wanaweza kuwa sahihi au si sahihi, wanaweza kuwa wanatumia njia sahihi kuzungumzia hilo lakini pia wanaweza kuwa wanatumia njia ya kuumiza na kukatisha tamaa ila yote kwa yote hizo ni hisia ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi kwani pengine yapo mawili matatu yanayofaa katika safari ya kuukwamua muziki wa dansi.

    Kwangu mimi naamini muziki wa dansi haujafa bali unazidi kukua kwa kasi ya ajabu kiasi cha kujipenyeza kwenye aina nyingine ya muziki kama vile bongo fleva, taarab na injili – ukifuatilia kwa makini aina hizo nyingine za muziki utagundua kuwa kwa zaidi ya asilimia 40 wanautegemea sana muziki wa dansi.
    Majuzi mwanangu wa kidato cha pili alinikuta natazama wimbo “Yarabi Nafsi” wa Mapacha Watatu katika laptop yangu kupitia YouTube, akashangaa sana na kuniuliza: “Hivi kumbe hata muziki wa bendi unapatikana You Tube?” Nikamjibu kwa kumhoji: “Kwanini ulifikiri haupatikani?”.
    Akanijibu: “Kwa sababu najua watu hawapendi muziki wa bendi za dansi, hawatapata viewers (watazamaji) wengi.” Kuthibitisha hilo akasogelea laptop yangu na kuangalia wimbo umepata watazamaji wangapi  akakuta 2781 akacheka.
    Mwanangu akaniambia: “Si umeona watazamaji hao, sasa nenda kwenye video za mastaa wa bongo fleva uangalie ‘viewers’ utakuta ni elfu 50 na kuendelea,”.
    Kwa bahati nzuri wakati dogo anayasema hayo nilikuwa na rafiki yangu aitwae Sakala Jr tukatazamana na kutabasamu kwa uchungu, ulikuwa ni ukweli unaoumiza kutoka kwa kijana mdogo ambaye ambaye anawakilisha sehemu ya kizazi kikubwa kinachoamini kuwa muziki wa dansi kupitia bendi zetu haukubaliki.
    Na ni hapo ndipo ninapojiuliza je bendi zetu zinajua kuwa zinahitaji kuzalisha mashabiki wapya kwa maana ya kizazi kipya? Mashabiki wanazeeka kiasi kwamba inafika wakati watu wanashindwa kwenda kwenye kumbi za starehe, nani anaziba nafasi zao? Watangazaji na waandishi waliokuwa wakiunadi muziki wa dansi miaka 20 iliyopita leo hii hawapo tena – wengine wamestaafu, wengine wamefariki, wengine wamebadilishiwa majukumu na sasa zimekuja damu mpya. Je bendi zetu zimefanya juhudi za kuishawishi jamii mpya ya wana habari?
    Wanamuziki nao wanapotea mmoja mmoja huku wakikosa warithi – kila damu msanii mpya wa muziki anakimbilia kwenye bongo fleva na mbaya zaidi kila mmoja anataka kuwa mwimbaji. 
    Hakuna anayetaka kujifunza kupiga chombo chochote na haitashangaza miaka 20 ijayo Tanzania ikawa haina mpiga gitaa wala ngoma.
    Bendi zimekosa ubunifu wa kwenda na wakati, ziko bendi zinapiga aina ile ile ya muziki kwa zaidi ya miaka 10, 15 au 20 bila kujali kuwa soko la muziki linabadilika kila wakati na kwamba walilazimika kulifuata.
    Inauma sana unaposikiliza vipindi vya muziki wa kiafrika kama Weekend Bonanza, Afrika Kabisa, Afro Power, Buzuki, Tanzania Stars, Afro Rhythm na vingine vingi, vinapopiga nyimbo za wasanii wa bongo fleva badala ya muziki wa bendi kama ilivyotarajiwa na wengi. 
    Lakini utawalaumu vipi watangazaji na waandaji wakati bendi zetu hazitaki kubadilika, hazitaki kurekodi nyimbo mpya na wala hazitaki kujiuliza ni kwanini nyimbo binafsi za wasanii wao zinapata muda wa kutosha redioni huku za bendi zinadorora.
    Kama msanii wa bendi anaweza kutoa wimbo wake binafsi unaokidhi mahitaji ya soko na ukapigwa redioni. ni kwanini asifanye hivyo kwenye bendi yake? Ni wazi kuwa fikra zao hazikubaliki ndani ya bendi na hivyo wanaamua kutoka kivyao vyao. 
    Kumbi zinazidi kukauka mashabiki, watu wanakimbilia ‘club’ kucheza disco au muziki wa kizazi kipya, inafika wakati hata bendi zinazopiga bure kwenye bar hazipati mashabiki - hiyo ni dalili tosha kuwa muziki wa bendi za dansi unakufa na kama juhudi za kuzalisha mashabiki wapya hazitafanyika, basi ‘mauti’ kwa bendi zetu yatakuwa hayakwepeki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AYA 15 ZA SAID MDOE: MUZIKI WA DANSI BADO KUZIKWA TU, UMEKWISHAUAWA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top