• HABARI MPYA

  Alhamisi, Juni 30, 2016

  WARAKA WA MALINZI JUU YA MECHI YA YANGA NA TP MAZEMBE...

  "NDUGU WANAHABARI, Nimewakaribisha kuzungumza nanyi kuhusu hali isiyo ya kawaida iliyojitokeza katika uendeshaji wa mashindano ya kimataifa hususani ushiriki wa Klabu ya Young Africans katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup).
  Awali ya yote ninaomba nichukue fursa hii kuwapongeza wachezaji,benchi la ufundi pamoja na uongozi wa
  klabu ya Yanga chini ya Rais wao Bwana Yusuf Manji kwa mafanikio makubwa ambayo klabu yao imepata hadi kufikia hatua ya makundi katika kombe la Shirikisho la CAF.Kuvunjika koleo sio mwisho wa uhunzi,imani ya TFF ni kuwa pamoja na kupoteza mechi mbili za mwanzo hatua ya makundi Yanga bado inaweza kufanya vizuri na kuwa moja ya timu bora mbili katika kundi lao.
  Ndugu zangu,TFF ndicho chombo chenye jukumu la kuendesha , kuratibu na kusimamia mashindano yote ya kitaifa na kimataifa ndani ya Tanzania Bara. Ikumbukwe kwamba mashindano yote ya CAF na FIFA ndani ya Tanzania msimamizi wake ni TFF.Hii ni kwa mujibu wa Katiba ya FIFA ibara ya 67,Katiba ya CAF ibara ya 59 na Katiba ya TFF ibara ya 12.
  Mashindano yoyote ya kimataifa yanayofanyika nchini Tanzania au kuhusisha timu za Tanzania ni sharti kibali kiombwe na TFF. Hivyo na ushiriki wa Young Africans na Azam katika mashindano ya kimataifa msimu wa 2015/2016 ulikuwa na baraka za TFF.
  Mamlaka ya TFF katika mashindano ya ndani na ya kimataifa  ni pamoja na usimamizi wa maandalizi ya mchezo, usimamizi wa mapato,usimamizi na uhakiki wa haki za matangazo, usalama ndani na nje ya uwanja,usimamizi wa upelekaji taarifa CAF na FIFA nk  Hivyo kwa yeyote anayetaka kucheza mpira unaotambuliwa na FIFA, CAF, CECAFA na TFF ni sharti akubaliane na kutii mamlaka hizi. Pale ambapo Katiba hizi hazielezei moja kwa moja utaratibu wa uendeshaji wa mashindano husika basi moja kwa moja vyombo hivi vya mpira huchukua jukumu la kutoa mwongozo.
  TFF inaomba kuchukua fursa hii kuwaomba radhi wadau wote wa mpira na wapenzi wote wa mpira kwa kadhia yote  iliyotokea kutokana na kitendo cha klabu ya Yanga kutoa tangazo la watazamaji kuingia bure katika mchezo namba 107 Yanga vs TP Mazembe uliofanyika uwanja wa Taifa Jumanne tarehe 28 June 2016. Aidha TFF inachukua fursa hii kuvishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua walizochukua ili kuepusha maafa ambayo yangeweza kutokea. Tunaushukuru uongozi wa Wizara ya habari,utamaduni,sanaa na michezo kwa ushirikiano wa karibu  waliotupatia wakati wa kuelekea kwenye mechi hii.Shukrani za pekee kwa Mh Paul Makonda,Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kwa kufuatilia kwa karibu matukio yote yaliyohusisha mchezo huu na kuhakikisha unamalizika salama.
  Sasa ninaomba turejee  kwenye matukio yaliyozunguka maandalizi ya mechi hii.Young Africans, wakiwa na wawakilishi wao katika mkutano wa maandalizi wa Alhamisi Juni 23, 2016 kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam walitangaza juu ya kuchapisha tiketi 40,000 na wakatangaza na viingilio.TFF baada ya kikao hicho iliwajulisha CAF  juu ya jambo hili kama ilivyo ada. 
  Mkutano wa kawaida wa maandalizi ya mechi (pre match meeting) baina ya timu zote mbili,yaani Yanga na TP Mazembe ulifanyika tarehe 27 June 2016 katika ukumbi wa hoteli ya Coral Beach, Masaki jijini Dar es Salaam na  uliendeshwa na Mratibu Mkuu  wa CAF wa mchezo huo (General coordinator) , Sidio Jose Magadza – Raia wa Msumbiji.Ni katika kikao hiki Yanga walitamka kuwa wameamua kiingilio kitakuwa ni bure.Msimamizi wa CAF alikiambia kikao kuwa kama hayo ndiyo maamuzi ya Yanga watambue kuwa itakuwa ni kwa gharama zao.Aidha aliagiza watazamaji 40,000 tu ndio waruhusiwe kuingia uwanjani hata kama ni bure,hii ni kwa sababu za kiusalama.Hilo halikufanyika na badala yake uwanja ulijaa watu 60,000. Na kutokana na pilika pilika za watu kutaka kuingia uwanjani zilitokea vurugu ambazo ilibidi wanausalama wazitulize kwa nguvu.Hili nalo lilishuhudiwa na wawakilishi wa CAF na hatujui wameripoti vipi tukio hili.Ikumbukwe wajibu wa TFF, CAF na FIFA ni kuhakikisha mashindano yao yanafanyika kwa utulivu na amani bila kuathiri maisha ya watu,mali zao na miundombinu ya michezo.
  Ndugu zangu,ninaomba nihitimishe kwa kuzungumzia yafuatayo.
  1.                             Serikali kupitia msimamizi wa uwanja wa Taifa ambaye ni Wizara ya habari Utamaduni Sanaa na michezo tarehe 27 June 2016 iliandika barua TFF ikitoa kibali  cha uwanja kutumika kwa mechi ya Yanga vs TP Mazembe kwa masharti kuwa miundo mbinu ya uwanja isiathirike,tozo na maduhuli (entitlements) ya Serikali yalipwe na usalama wa watazamaji ulindwe.TFF inawasiliana na mamlaka husika ikiwemo Wizara,mamlaka ya mapato pamoja na CAF ili kujua ni kiasi gani wanatakiwa kulipwa.Hili likisha fahamika basi TFF itachukua jukumu lake kama msimamizi wa mpira nchini kuhakikisha kila mwenye kudai analipwa. 
  2.                             TFF inafuatilia kwa karibu kujua nini yatakuwa maamuzi ya CAF kutokana na ripoti za msimamizi na kamisaa wa mchezo  kuhusu matukio yaliyotokea nje ya uwanja kabla na wakati wa mechi.
  3.                             TFF itaendelea kufanya kila lililo katika uwezo wake kuhakikisha Yanga inaendelea kufanya vizuri kwenye mashindano haya kwani bado ina nafasi.
  4.                             Siku zote TFF imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha mchezo wa mpira unachezwa katika eneo salama.Hivyo kuanzia sasa jukumu la kusimamia michezo ya kimataifa litakuwa linaratibiwa kwa karibu zaidi na TFF ikiwa ni pamoja na mapokezi ya timu,maofisa,kuangalia malazi kama yako sahihi,usalama,maamuzi kuhusu viingilio na uuzaji wa tiketi,usafiri wa ndani,viwanja vya mazoezi nk.
  Ninaomba nimalizie kwa kuwatakia tena ndugu zetu Waislam ibada njema ya Mwezi Mtukufu wa  Ramadhan,niitakie pia kila la kheri timu yetu ya Serengeti Boys ushindi katika mchezo wa marudianao Jumamosi dhidi ya Seychelles. Michezo ni furaha,michezo ni afya.
  Ahsanteni kwa kunisikiliza,".
  (Imetolewa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi Juni 30, 2016 mjini Dar es Salaam)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WARAKA WA MALINZI JUU YA MECHI YA YANGA NA TP MAZEMBE... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top